SYRIA-UTULIVU-MAXUNGUMZO

Utulivu Syria kabla ya kuanza kwa mazungumzo Alhamisi

Magari yakiendeshwa usiku mitaani mjini Aleppo Aleppo, Machi 5, 2016.
Magari yakiendeshwa usiku mitaani mjini Aleppo Aleppo, Machi 5, 2016. AFP

Mazungumzo kuhusu ufumbuzi wa kisiasa kutokana na vita vinavoendelea nchini Syria yataanza Alhamisi hii wakati ambapo maeneo yanayohusu mkataba wa usitishwaji wa mapigano yameonekana kuwa shwari Jumapili hii.

Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo haya mjini Geneva, chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa, yatakuwa ya kwanza tangu mkataba wa usitishwaji wa mapigano kati ya waasi na serikali kuanza kutekelezwa tarehe 27 Februari mwaka huu, ingawa kwa sasa upinzani, ambao ni dhaifu katika uwanja wa vita, umekua ukisita kushiriki katika mazungumzo hayo.

Katika maeneo yanayohusu mkataba wa usitishwaji wa mapigano yalioafikiwa kati ya kati ya Urusi na Marekani, "yameonekana shwari Jumapili hii tangu kuanza kutekelezwa mkataba wa usitishwaji wa mapigano," Mkurugenzi wa shirika la haki za binadamu (OSDH), Abdel Rahman, ameliambia shirika la habari la Ufaransa la AFP. Shirika hili lina mtandao mpana wa vyanzo kupitia nchi nzima ya Syria.

Utulivu umeshuhudiwa katika zaidi ya mikoa hii, ispokua tu roketi kadhaa za Al-Nosra Front, na kundi la Islamic State, makundi ambayo yametengwa katika mazungumzo hayo, na waasi wa kundi la Kikurdi zimerushwa katika kitongoji kimoja kaskazini mwa mji wa Aleppo. Milipuko hiyo ilisababisha vifo vya watu watatu, kwa mujibu wa OSDH na waasi wa Kikurdi.

Mashambulizi makali pia yameendelea katika maeneo yanayoshikiliwa na makundi ya Islamic State na al-Nosra Front (tawi la Al Qaeda nchini Syria), yaliotengwa katika mazungumzo yanayotazamiwa kuanza Alhamisi Machi 10.

Kwa mujibu wa Bw Abdel Rahman, idadi ya wastani ya vifo kwa siku miongoni mwa raia "imepungua kwa 90%" katika kipindi hiki cha usitishwaji mapigano ikilinganishwa na kipindi cha nyuma. Idadi ya vifo imeshuka kwa 80% kwa askari na waasi, ameongeza Bw Abdel Rahman.

Siku chache kabla ya mazungumzo hayo, ambayo yamepangwa kuanza Alhamisi kwa mujibu wa mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura, upinzani bado unasita kushiriki mazungumzo hayo.