YEMENI-HOUTHI-USHIRIKIANO

Waasi wa Kishia ziarani Saudi Arabia kujadili amani Yemen

Waasi wa Kishia wa Houthi katika mji mkuu Sanaa, Februari 10, 2015.
Waasi wa Kishia wa Houthi katika mji mkuu Sanaa, Februari 10, 2015. REUTERS/Khaled Abdullah

Ujumbe wa waasi wa Kishia wa Houthi nchini Yemen wako nchini Saudi Arabia kwa mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro nchini Yemen, wamesema Jumanne hii viongozi wawili wa waasi.

Matangazo ya kibiashara

Ziara hii ni ya kwanza tangu kuanza kwa mgogoro, mwaka mmoja sasa, kati ya waasi wa Kishia na majeshi ya serikali yanayosaidiwa na muungano wa Kiarabu unaoongozwa na Saudi Arabia.

Ujumbe huu wa waasi wa Kishia unaongozwa na Mohamed Abdel-Salam, msemaji mkuu wa kundi hili la waasi na mshirika wa karibu wa kiongozi wa kundi la waasi, Abdel-Malek al Houthi, viongozi hao wameongeza.

Abdel-Salam tayari aliongoza ujumbe wa waasi wa Houthi katika mazungumzo nchini Oman, mazungumzo ambayo yalifungua njia kwa mazungumzo chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa mwaka jana nchini Uswisi.

ziara ya ujumbe huu ilianza Jumatatu, kwa mwaliko wa viongozi wa Saudi, baada ya wiki moja ya kukutana kwa maandalizi yaliyofanywa kwa siri, viongozi hao wawili wamebainisha.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia na muungano wa Kiarabu bado hawajahibitisha kuwepo kwa ujumbe wa waasi wa Houthi nchini Saudi Arabia.