URUSI-SYRIA-USHIRIKIANO-USALAMA

Urusi yaanza zoezi la kuwaondoa askari wake kutoka Syria

Rais wa Urusi Vladimir Putin (kushoto) katika Ikulu ya Kremlin Moscow, Machi 14, 2016.
Rais wa Urusi Vladimir Putin (kushoto) katika Ikulu ya Kremlin Moscow, Machi 14, 2016. MIKHAIL KLIMENTYEV/SPUTNIK/AFP

Urusi imeanza zoezi la kuwaondoa vifaa vyake vya kijeshi kutoka Syria, Waziri wa Ulinzi wa Urusi amesema Jumanne hii saa chache baada ya Rais Vladimir Putin kutangaza Jumatatu hii usiku kwamba sehemu kubwa ya askari wa Urusi wataondolewa nchini Syria, na kurejea Urusi.

Matangazo ya kibiashara

"Mafundi wameanza kuandaa ndege kwa ajili ya safari za muda mrefu wakielekea katika kambi zao za jeshi nchini Urusi wakitokea Syria," wizara ya Ulinzi imebaini katika taarifa yake, ikiongeza kwamba wanajeshi wameanza kuandaa kupakia vifaa vya kijeshi ndani ya ndege.

Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Syria Bashar al-Assad walikubaliana kwa njia ya simu Jumatatu hii usiku juu ya uondoaji wa majeshi ya Urusi kutoka Syria,. Ikulu ya Urais wa Urusi (Kremlin) imebaini kwamba nchini Syria watasalia tu wanajeshi wa anga.

"Rais wa Urusi amesema kuwa operesheni kuu zilizoombwa kwa vikosi vya kijeshi zimekamilika. Suala lililoafikiwa ni uondoaji wa sehemu kubwa ya kikosi cha wanajeshi wa anga wa Urusi," Kremlin imesema katika taarifa yake, huku ikiongeza kuwa idadi ndogo ya wanajeshi wa anga itaendelea kuwepo kwa kuimarisha utekelezaji wa mkataba wa usitishwaji wa mapigano.

Itafahamika kwamba mazungumzo kati ya serikali ya Syria na Upinzani yenye lengo la kumaliza mgogoro nchini Syria yalianza Jumatatu hii katika mji wa Geneva chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa, lakini hatima ya Rais Bashar al-Assad inaweza kuzorotesha mchakato wa amani.

Msimamizi wa mazungumzo hayo, Staffan de Mistura, Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, amesema kuwa "suala mama" ni kufikiwa makubaliano kuhusu mabadiliko ya kisiasa. "Tupo katika wakati wa ukweli," ameongeza katika mkutano na waandishi wa habari katika utangulizi wa mkutano wake na kiongozi wa ujumbe wa serikali ya Damascus, Bashar Bashar al-Jaafari.

Baada ya mkutano huo wa kwanza, ambao umedumu zaidi ya saa moja katika Jumba la Mataifa, Bw De Mistura ameeleza "aliruhusu kufafanua masuala kadhaa, hususan masuala ya kiutaratibu." "Mkutano ujao (na serikali) Jumatano asubuhi utajikita kwenye ajenda, ambayo ni kama mnavyojua ile iliyowekwa na azimio 2254," De Mistura ameongeza.

Waraka huu, iliyopitishwa mwezi Desemba na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, unatoa uundwaji wa taasisi ya mpito nchini Syria ndani ya miezi 6 na uchaguzi ndani ya miezi 12

Kwa upande mwingine, Bw Jaafari amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba mkutano alikuwa "mzuri na wenye lengo la kujenga". Amesema alimpa Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa "mambo ya msingi kwa ufumbuzi wa kisiasa," lakini bila kutoa maelezo.

"Tunataka mazungumzo kati ya wadau wote nchini Syria, lakini bila masharti," ameongeza Bw Jaafari, balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa, akimaanisha madai ya upinzani ambao unadai kuondoka madarakani kwa Rais Assad, akiwa ameuawa au hai kabla ya ufumbuzi wowote wa kisiasa.