Serikali ya Syria yadhibiti Palmyra, ushindi mkubwa dhidi IS
Imechapishwa:
Jeshi la Syria likisaidiwa na mshirika wake Urusi wamelikabili kundi la Islamic State na kupata ushindi mkubwa Jumapili hii, kwa kuuteka mji wa kale wa Palmyra, na kuahidi kulitimua kundi hili la kijihadi katika ngome zake kuu nchini Syria.
Huu ni ushindi muhimu zaidi wa serikali dhidi kundi la IS tangu Urusi kuingilia kijeshi mwishoni mwa mwezi Septemba 2015 katika mgogoro wa Syria. Urusi ni mshiika wa karibu wa Rais Bashar al-Assad.
Baada ya kuuteka mji wa Palmyra, vikosi vya serikali vinapania kuwatimua wapiganaji wa kundi la Islamic State katika kijiji cha Al-Alianiyé, kilomita 60 kusini mwa Syria, ili kuchukua udhibiti wa eneo la jangwa la Syria na kuelekea kwenye mpaka na Iraq, unaodhibitiwa kwa kiasi kikubwa na wapiganaji wa kijihadi.
Akizungumza mbele ya wabunge wa Ufaransa ziarani Damascus, Bw Assad ameuelezea ushindi huu kama "kazi muhimu ya ukombozi wa mji wa Palmyra (katikati)", mji wa kale wa zaidi ya miaka 2,000, ambapo magofu yake yaliwekwa katika mali za kimataifa za shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Huu ni "ushahidi mpya na ufanisi wa mkakati wa jeshi la Syria na washirika wake katika vita dhidi ya ugaidi, ikilinganishwa na ukosefu wa umakini wa muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani" dhidi IS, Bashar Al Assad, ameongeza.
Siku 20 za mapigano zimegharimu maisha ya wanajihadi 400, "idadi kubwa ya vifo kwa kundi la IS katika vita moja tangu kuibuka kwake". Vita ambavyo vilizuka tangu mwaka 2013, kwa mujibu wa shirika la Haki za binadamu nchini Syria (OSDH ). Askari 188 wa serikali wameuawa katika vita hivyo.