IRAQ-IS-MASHAMBULIZI-USALAMA

Watu 3 wauawa na 22 kujeruhiwa katika shambulizi Baghdad

Wairaq wakisafisha eneo la shambulizi la kujitoa mhanga lililodaiwa kutekelezwa na kundi la Islamic State ambalo limesababisha vifo vya watu watatu na 22 kujeruhiwa katika Tayaran Square, Baghdad Machi 29, 2016.
Wairaq wakisafisha eneo la shambulizi la kujitoa mhanga lililodaiwa kutekelezwa na kundi la Islamic State ambalo limesababisha vifo vya watu watatu na 22 kujeruhiwa katika Tayaran Square, Baghdad Machi 29, 2016. AFP/SABAH ARAR

Mshambuliaji wa kujitoa mhanga amelipua mkanda wake uliokua umejaa vilipuzi katikati mwa mji wa Baghdad Jumanne hii, na kusababisha vifo vya watu 3 na kuwajeruhi 22, shambulizi ambalo limedaiwa kutekelezwa na kundi la Islamic State (IS).

Matangazo ya kibiashara

Shambulizi hili limewalenga wafanyakazi waliokusanyika katika Tayaran Square, eneo linalotembelewa na watu wengi katika mji mkuu wa Iraq, kwa mujibu wa vyanzo vya hospitali na vya usalama.

Katika taarifa yake iliyorushwa hewani katika mitandao yake, kundi la Islamic State limedai kuwa limetekeleza shambulio hilo, likithibitisha kwamba limekua limelenga vikosi vya kijeshi vya Kishia.

Kundi la Islamic State lenye kutoka jamii ya Masuni wenye msimamo mkali lilidhibiti mwezi Juni mwaka 2014 sehemu kubwa ya ardhi ya Iraq lakini tangu wakati huo wamepoteza maeneo mengi kufuatia mashambulizi ya vikosi vya jeshi vya Iraq vinavyosaidiwa na wanamgambo wa Kishia na ndege za muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani.

Wanajihadi, ambao wanadhibiti sehemu kadhaa ya jimbo la magharibi la Al Anbar, wanapatikana kilomita hamsini magharibi mwa mji wa Baghdad lakini wanaendelea kutekeleza mashambulizi katika mji mkuu na viunga vyake.