YEMEN-MAZUNGUMZO

Serikali ya Yemen yasitisha mazungumzo na waasi

Ismail Ould Cheikh Ahmed, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Kuwait Aprili 26, 2016.
Ismail Ould Cheikh Ahmed, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Kuwait Aprili 26, 2016. AFP

Serikali ya Yemen imetangaza Jumapili hii kwamba imesitisha "mazungumzo ya moja kwa moja" na waasi wa Kishia na washirika wao nchini Kuwait baada ya waasi kudhibiti kambi ya jeshi katika ukiukaji wa mkataba tete nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Ujumbe wa serikali, hata hivyo, utabaki nchini Kuwait na kuendelea na mazungumzo yasio kuwa ya moja kwa moja kupitia mpatanishi wa Umoja wa Mataifa Ismail Ould Cheikh Ahmed, afisa mwandamizi wa serikali ameliambia shirika la habari la AFP.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa alifanikiwa siku ya Jumamosi kwa kuandaa mazungumzo ya moja kwa moja, ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mazungumzo ya Aprili 21, kwa mujibu wa wajumbe wa serikali katika mazungumzo hayo.

"Tumeamua kusitisha mazungumzo ya moja kwa moja na ujumbe wa waasi ili kupinga dhidi ya kuendelea kukiuka mkataba wa usitishwaji wa mapigano" uliotangazwa Aprili 11, na "tunatoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kwa umakini ili kumaliza ukiukwaji huu unaotishia kudhoofisha mazungumzo ya amani, " ujumbe wa serikali umeongeza.

Kwa mujibu wa ujumbe huo, "mawasiliano yataendelea na mpatanishi wa Umoja wa Mataifa pamoja na wadhamini" wa mchakato wa amani.

Uamuzi huu unakuja baada ya waasi wa Kishia wa Houthi kudhibiti kambi kubwa ya jeshi katika eneo la kaskazini.

Kambi ya kijeshi ya Al-Amaliqa katika jimbo la Amrane, limedhibitiwa na maelfu ya waasi wa Kishia wa Houthi na washirika wao, kwa mujibu wa vyanzo vya kijeshi.