SYRIA-USALAMA-SIASA

Kundi la Kimataifa linalounga mkono Syria kukutana Mei 17

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova, Moscow Januari 26, 2016.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova, Moscow Januari 26, 2016. AFP

Mkutano wa kundi la Kimataifa linalounga mkono Syria (GISS), utakaoongozwa na Urusi pamoja na Marekani, umepangwa kufanyika Mei 17 katika mji wa Vienna, Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imetangaza Jumanne hii.

Matangazo ya kibiashara

"Tumeafikiana tarehe 17 Mei," msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Urusi, Maria Zakharova, amesema akijibu swali la shirika la habari la AFP kuhusu mkutano wa GISS (nchi 17 na mashirika matatu ya kimataifa) wa Mei 17 katika mji wa Vienna na ushiriki wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov.

Mkutano huu unawadia wakati Moscow na Washington waliahidi "kuongeza mara dufu jitihada zao" kufikia ufumbuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Syria.

Marekani na Urusi wamechangia kwa kiasi kikubwa kwa kurejesha amani katika baadhi ya maeneo ya nchi ya Syria.

Hali ya utulivu imekua ikishuhudiwa katika jimbo na mji wa Aleppo nchini Syria, licha ya makabiliano madogo madogo kati ya jeshi la serikali na waasi, baada ya Marekani na Urusi kufikia mwafaka wa kusitisha mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea kwa zaidi ya wiki mbili na kusababisha mamia ya watu kupoteza maisha.