Moscow yatoa wito wa "kusitishwa mapigano" katika mikoa miwili Syria
Imechapishwa:
Urusi imetoa wito wa masaa 72 ya kusitisha mapigano kuanzia Alhamisi hii, Mei 26 katika mikoa miwili ya Syria ambapo mapigano yanaendelea licha ya mkataba wa kusitisha mapigano ulioanza kutekelezwa Februari 27.
Moscow imetoa wito wa "kusitishwa kwa mapigano" kwa masaa 72 katika mikoa miwili ilio karibu na mkoa wa Damascus ili kurejesha hali ya utulivu katika maeneo hayo. Mikoa hiyo ni pamoja na Daraya na Ghouta Mashariki. Wito huu wa Urusi wa kusitisha mapigano unakuja wakati ambapo Marekani imeiomba Urisi kuishinikiza serikali ya Syria ili kusitisha mashambulizi katika mkoa wa Aleppo na pembezoni mwa mji wa Damascus.
Wakati huo huo, Wizara ya mambo ya Nje ya Marekani inasema kuwa iliwashinikiza washirika wake miongoni mwa makundi ya waasi kuendelea kuheshimu mkataba wa usitishwaji mapigano.
Vitisho vya Urusi
Serguei Kouralenko, mkurugenzi wa kituo cha kuratibu cha Urusi nchini Syria, pia ametolea wito upinzani nchini Syria kuondoka katika maeneo yanayodhibitiwa na wanajihadi wa kundi la Al-Nosra Front. Amesema makundi ya waasi mashariki mwa mkoa wa Ghouta Mashariki na katika vitongoji vya mkoa wa Damascus yamejikusanya na yanajiandaa hatimaye kuendesha mashambulizi makubwa. Pia amesema kuwa kundi la al-Nosra Front limekusanya wapiganaji 6000 kwa lengo la kuanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya mji wa Aleppo.
Urusi imetishia kuanzisha mashambulizi dhidi ya makundi ya waasi ambayo inaona hayaheshimu mkataba wa usitishwaji mapigano. Urusi pia imeipendekeza Marekani kuendesha mashambulizi ya pamoja dhidi ya makundi ya wanajihadi, pendekezo ambalo limekataliwa na Washington.