SYRIA

Mji wa Aleppo waendelea kushambuliwa na vikosi vya Serikali ya Syria

Moshi ukiwa umetanda kwenye eneo kubwa la mji wa Aleppo baada ya kushambuliwa
Moshi ukiwa umetanda kwenye eneo kubwa la mji wa Aleppo baada ya kushambuliwa REUTERS/Abdalrhman Ismail

Mashambulizi ya anga yaliyofanywa na vikosi vya Serikali kwenye mji wa Aleppo hii leo, yameua watu wanaokadiriwa kufikia 16, limesema shirika moja la waangalizi wa haki za binadamu. 

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa waangalizi hao, mashambulizi hayo yameuahiribu kwa sehemu kubwa mji wa Aleppo na hasa kwenye maeneo yanayokaliwa na wapiganaji wa Islamic State.

Vikosi vya Serikali vinadaiwa kutumia mabomu ya kutawanyika kwenye ngome za wapiganaji wa ISIL, mabomu ambayo hata hivyo jumuiya ya kimataifa imekuwa ikipinga kutumiwa dhidi ya binadamu.

Shirika moja la kutetea haki za binadamu, limesema kuwa watu 9 waliuawa kwenye mji wa Qaterji na wengine wawili waliuawa kwenye mji wa jirani wa Mayassar, kaskazini mwa jiji la Aleppo.

Mmoja wa wakaazi wa mji wa Aleppo akiwa amembeba mtoto aliyejeruhiwa
Mmoja wa wakaazi wa mji wa Aleppo akiwa amembeba mtoto aliyejeruhiwa REUTERS/Abdalrhman Ismail

Mamia ya raia wameripotiwa kunaswa kwenye mapigano ndani ya mji wa Aleppo na hawana sehemu ya kutokea kwakuwa maeneo mengi yamezingirwa na ama vikosi vya Serikali ama wapiganaji wa Islamic State.

Vikosi vya uokoaji vimeonekana vikiingia kwenye mji huo kujaribu kuwaokoa watu walionaswa kwenye vifusi vya majengo yaliyoanguka baada ya kushambuliwa na mabomu, huku watoto na wanawake ndio wakionekana kuathirika kwa asilimia kubwa.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoafikiwa na Urusi pamoja na Marekani, mwezi February mwaka huu, yamekiukwa kwa sehemu kubwa karibu kila siku kwenye mji wa Aleppo, ambako vikosi vya Serikali na waasi wameendelea kupigana kuwania umiliki wa mji huo toka mwaka 2012.

Zaidi ya watu laki 2 wanaishi kwenye maeneo mengi ya mji wa Aleppo na hasa kwenye maeneo yanayokaliwa na waasi na njia kuu iliyokuwa inatumiwa kuwafikia wananchi kutoa misaada ndio inashuhudia mapigano makali yasiyosimama.