SYRIA-BASHAR AL ASSAD

Syria: Assad amteua Waziri Mkuu mpya

Waziri Mkuu mpya wa Syria, Imad Khamis.
Waziri Mkuu mpya wa Syria, Imad Khamis. STR / AFP

Jumatano wiki hii Rais wa Syria alimteua Waziri Mkuu mpya, Imad Khamis, akichukua nafasi ya Wael al-Halqi, ambaye alihudumu kwenye wadhifa huo tangu mwezi Agosti 2012. Uteuzi huu unakuja baada ya uzinduzi wa Bunge lililotokana na uchaguzi ulioandaliwa na serikali, mwezi Aprili katika maeneo yaliyo chini ya utawala wake.

Matangazo ya kibiashara

Uchaguzi ambao ulishutumiwa na jumuiya ya kimataifa na upinzani nchini Syria. Waziri Mkuu mpya atasimamia uchumi ambao unaonekana kudidimia.

Imad Khamis kutoka jamii ya Masuni, mzaliwa wa mkoa wa Damascusi, ni mfuasi wa chama tawala cha BAAS tangu alipokua na umri wa miaka 16. Mhandisi huyu, mwenye umri wa miaka 54 ni mmoja wa wataalam bora katika nchi hiyo katika nyanja ya umeme. Sekta ambayo imeathirika vibaya na vita, ikiwa ni pamoja na uzalishaji ulio chini kwa karibu 60% tangu mwaka 2011.

Imad Khamis itakuwa na kazi ngumu ya kusimamia uchumi unaoonekana kudidimia katika nchi isiyokua na rasilimali. Serikali ya Bashar Al Assad inashikilia maeneo yenye wakazi 60% kwa jumla ya wananchi milioni 23, wakiwemo wakimbizi wa ndani milioni saba.

Waziri Mkuu mpya pia atapambana na kupanda kwa mfumuko wa bei, kushuka kwa sarafu ya Syria na uhaba wa petroli na mafuta katika nchi inayokabiliwa na rushwa.

Mchakato unaojulikana kama maridhiano, ambayo ina idara maalum, pia ni sehemu ya majukumu yake. Hata hivyo, jeshi, vyombo vya usalama na Wizara ya Mambo ya Nje haviko chini ya mamlaka yake.