LEBANON-IS

Watu 5 wauawa Bekaa katika mfululizo wa mashambulizi

Askari wa jeshi la Lebanon wakitoa ulinzi katika eneo la mashambulizi, baada ya mashambulizi ya kujitoa mhanga Juni 27 katika kijiji cha Qaa, Bekaa.
Askari wa jeshi la Lebanon wakitoa ulinzi katika eneo la mashambulizi, baada ya mashambulizi ya kujitoa mhanga Juni 27 katika kijiji cha Qaa, Bekaa. REUTERS/Hassan Abdallah TPX IMAGES OF THE DAY

Watu watano wameuawa na wengine 15 wamejeruhiwa mapema Jumatatu asubuhi katika mfululizo wa mashambulizi ya kujitoa mhanga katika kijiji cha mashariki mwa Libanon karibu na mpaka na Syria, viongozi wametangaza.

Matangazo ya kibiashara

Mfululizo huu wa milipuko umetokea katika kijiji cha Qaa, kinachokaliwa na watu kutoka jamii ya Wakristo, katika jimbo la Bekaa, karibu na mpaka na Syria.

Mashambulizi haya manne ya kujitoa mhanga yametokea kwa muda wa dakika chache katika kijiji cha Qaa, katika jimbo la Bekaa. Mshambuliaji wa kwanza wa kujitoa mhanga amelipua mkanda wake uliokua umejaa vilipuzi katika eneo la kituo cha ukaguzi cha jeshi la Lebanon. Wakati watu walipokua wakikimbia kuwaokoa waathirika, mgaidi mwingine alijilipua, akifuatiwa na washambuliaji wawili wakujitoa mhanga.

Hakuna kundi hata moja ambalo limeshatangaza kuhusika na mfululizo huu wa mashambulizi, lakini kwa vyovyote vile kundi la Islamic State linanyooshewa kidole kwa kuhusika na tukio hilo. Kwa sababu wanajihadi wa kundi hili linaloongozwa na Abu Bakr al-Baghdadi, wanaendesha mara kwa mara harakati zao katika jimbo hili lenye milima, kunakopatikana kijiji cha Qaa.

Wakati huo huo wa mashambulizi ya Qaa,kundi la Islamic State limekua likiendesha mashambulizi kababmbe dhidi ya kijiji cha Brital kinachokaliwa na watu kutoka jamii ya Mashia, lakini wapiganaji wa kundi hili walirudishwa nyuma na jeshi la Lebanon baada ya mapigano makali. Mapigano kati ya jeshi la Lebanon na kundi la Islamic State yanatokea mara kwa mara kwenye umbali wa kilomita 50 kwenye mpaka wa Lebanon na Syria, katika eneo kulikojengwa makambi kadhaa ya wakimbizi wa Syria.