YEMEN-USALAMA

Hali ya usalama yaendelea kuwa tatanishi Yemen

Vikosi vya serikali ya Yemen, Aden.
Vikosi vya serikali ya Yemen, Aden. AFP

Hali ya kiusalama imeendelea kutisha nchini Yemen baada ya watu 80 kuuawa na wengine 37 kujeruhiwa ndani ya massa 24. Watu hao wameuawa katika mashambulizi ya anga na mapigano yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa yanaendelea kwa mwendo wa kinyonga, na hivyo kusababisha hali ya mkanganyiko.

Vifo hivi vya watu 80 ni pamoja na watu 42 waliouawa Jumatatu hii katika mfululizo wa mashambulizi dhidi ya wanajeshi, iyaliyodaiwa kutekelezwa na wanajihadi wa kundi Islamic State (IS) katika ngome ya zamani ya hasimu wake Al Qaeda kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Hali ya usalama imedorora tangu wiki iliyopita nchini Yemen, wakati ambapo mazungumzo yaliyoanza tangu Aprili 21 mwaka huu nchini Kuwait kati ya serikali ya Yemen na waasi wa Kishia wa Houthi yanatazamiwa kusitishwa wiki ijayo kwa ajili ya Siku kuu ya Eid al-Fitr inayoashiria mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, kwa Waislamu.

Akiwa ziarani nchini Kuwait siku ya Jumapili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alitoa wito kwa pande zinazohusika katika mgogoro nchini Yemen kushirikiana na mjumbe wake nchini humo kwa "kukubaliana kwa kanuni moja na kufikia makubaliano ya kudumu" kwa kumaliza miezi 15 ya vita.