WAISLAMU

Waislamu washerehekea sikukuu ya Eid al Fitr

Waislamu nchini Qatar
Waislamu nchini Qatar http://static.qatarliving.com/

Waislamu kote duniani wanaadhimisha sikukuu ya Eid al Fitr kutamatisha mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Matangazo ya kibiashara

Leo ni mapumziko katika mataifa mbalimbali duniani hasa yale ya Kiislamu kama Saudi Arabia .

Nchini Iraq, raia wa nchi hiyo bado wanaendelea kuomboleza baada ya shambulizi la bomu kusababisha vifo vya zaidi ya watu 200 mjini Bagdad.

Ripoti zinasema kuwa idadi ya vifo imeongeza na kufikia 250 kufikia siku ya Jumatano.

Nchini Saudi Arabia, maelfu ya mahujaji wapo katika miji mitakatifu ya Mecca na Medina kuadhimisha siku ya kwanza ya Eid al Fitr.

Wiki hii watu wanne walipoteza maisha mbele ya Msikiti wa Mtume Mohammed mjini Medina baada ya kujilipua, shambulizi ambalo lililaaniwa na viongozi wa Kiislamu nchini humo.

Mataifa mengine ambayo sherehe hizi zimepamba moto ni pamoja na Yemen, Indonesia na Ufilipino.

Hali ni vivyo hivyo barani Afrika, nchini Kenya hasa Pwani ya nchi hiyo usalama umeimarishwa kuhakikisha kuwa Waislamu na watalii wengine wanakuwa salama.

Nchini Tanzania mamia ya waumini walijitokeza katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam kuadhimisha siku hii.

Viongozi wa dini hiyo hutumia siku hii kuhubiri amani na kulaani ugaidi.

Siku hii Familia zinashereherekea pamoja kwa kula pamoja na kuwatembelea watu wasiojiweza.