UN-SYRIA

UN yachelewesha mpango wa kuhamisha watu Aleppo

Hofu ya mapigano imetanda jimboni Aleppo na kuisababisha UN kuchelewesha mpango wa uokozi
Hofu ya mapigano imetanda jimboni Aleppo na kuisababisha UN kuchelewesha mpango wa uokozi AMEER ALHALBI / AFP

Wasiwasi juu ya usalama umeulazimu umoja wa mataifa kuchelewesha mpango wa kuhamisha watu kutoka mjini Aleppo wakati huu Urusi ikiongeza muda wa usitishwaji wa mapigano kwa siku ya tatu leo jumamosi.

Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Moscow imesema inaongeza muda wa usitishwaji wa mashambulizi kwa kuzingatia sababu za kibinadamu hadi saa kumi za jioni kwa saa za Syria.

Hata hivyo hakukuwa na dalili kwamba raia au waasi walizingatia wito wa kuondoka huku Damascus na Moscow zikishutumu wapiganaji waasi kwa kuzuia uhamishwaji.

Huko Geneva, baraza la haki la umoja wa mataifa limeitisha uchunguzi maalum kuhusu ghasia za Aleppo.

Mashariki mwa  Aleppo,eneo ambalo waasi walidhibiti mnamo mwaka 2012,limekuwa chini ya ulinzi wa jeshi tangu katikati mwa mwezi Julai na kukabiliwa na mashambulizi ya mabomu kutoka kwa serikali na mshirika wake Urusi tangu septemba 22 zilipoanzishwa harakati za kukomboa mji wote.

Takribani watu mia tano wameuawa,zaidi ya robo yao wakiwa watoto tangu kuanza kwa mashambulizi na kushuhudia majeruhi takribani elfu mbili.