IRAQ-SYRIA-ISIL

UN: ISIL inatumia raia kama kinga kwenye mji wa Mosul

Kundi la wapiganaji wa kiislamu wa Islamic State nchini Iraq pamoja na wale wa Levant, wameripotiwa kutumia maelfu ya raia kama "kinga" ya mashambuzili kwenye mji wa Mosul, ambako wanajeshi wa Serikali wanaendelea na operesheni za kuuchukua mji huo wa pili kwa ukubwa.

Wakimbizi raia wa Syria na Iraq wakiwa wanalindwa na wanajeshi wa Serikali baada ya kuwakimbia wapiganaji wa ISIL, October 28, 2016.
Wakimbizi raia wa Syria na Iraq wakiwa wanalindwa na wanajeshi wa Serikali baada ya kuwakimbia wapiganaji wa ISIL, October 28, 2016. REUTERS/Rodi Said
Matangazo ya kibiashara

Ofisi ya mkuu wa tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa, imesema kwenye taarifa yake kuwa, imepokea taarifa kuwa zaidi ya watu 200 wameuawa baada ya kukataa kutii amri ya wapiganaji hao na wengine kwakuwa walikuwa na uhusiano na vikosi vya Serikali.

Tume hiyo imeongeza kuwa "taarifa za kusikitisha" zinaonesha kuwa wapiganaji wa ISIL wamekuwa wakiwalazimisha maelfu ya raia kutoka majumbani mwao na kuwatumia kama ngao.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wapiganaji wa ISIS wanatumia mbinu chafu za kuwatumia raia kama kinga kwenye baadhi ya maeneo, ili kuwafanya wanajeshi wa Serikali washindwe kutekeleza mashambulizi dhidi ya ngome zao.

Msemaji wa tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa, wapiganaji hao wanawatumia watoto, wasichana na wanawake kama kinga, huku wakiwalazimisha vijana wakiume kushika bunduki kukabiliana na vikosi vya Serikali.

Shamdasani amesema kuwa, watu wanaokadiriwa kufikia 232, wengi ambao walikuwa ni wanajeshi wa Serikali, wameripotiwa kupigwa risasi Jumatano ya tarehe 26.

Inaarifiwa kuwa wapiganaji hao wanafanya kila linalowezekana kuwatisha raia ambapo wamekuwa wakiua mtu yeyote ambaye atakuwa anaweka upinzani dhidi yao.

Katika hatua nyingine, wapiganaji wanaosaidiana na wanajeshi wa Serikali, wameanzisha operesheni kubwa kulenga mji wa Tal Afar, ambao bado uko chini ya wapiganaji wa Islamic State.

Vikosi vya Hashed al-Shaab wanaoungwa mkono na watu wa makabila ya kishia, wamekuwa wakipigana sambamba na wanajeshi wa Serikali kwenye operesheni ya kuuchukua tena mji wa Mosul kutoka kwa ISIL.

Vikosi hivyo vimeanza operesheni hii vikitokea upande wa Syria ambako wapiganaji wa Islamic State wanaelezwa kukimbilia.