IRAQ-IS

Majeshi ya Iraq yaingia Mosul

Operesheni dhidi ya kundi la Islamic State kusini mwa mji wa Mosul, Oktoba 31, 2016.
Operesheni dhidi ya kundi la Islamic State kusini mwa mji wa Mosul, Oktoba 31, 2016. REUTERS/Stringer

Kwa mara ya kwanza majeshi ya Iraq yamefanikiwa kuingia katika baadhi ya maeneo ya mashariki mwa mji wa Mosul, huku yakijaribu kuwatimua wanamgambo wa kundi la Islamic State kutoka mji huo ulio Kaskazini mwa nchi.

Matangazo ya kibiashara

Vikosi maalum dhidi ya ugaidi viliweka chini ya himaya yao eneo la Kukjali kunakopatikana jengo la runinga ya taifa saa kadha baada ya kufanya mashambulizi eneo hilo.

Karibu wanajeshi 50,000 wa Iraq, wapiganaji wa Kikurdi na wale kutoka Jamii ya Sunni na Shia wanashiriki kwenye mapigano hayo yanayodumu sasa wiki mbili, kuwatimua wapiganaji wa kundi la Islamic State kutoka ngome yao kuu na ya mwisho nchini Iraq.

Vikosi hivyo vilichukua udhibiti wa kijiji cha Bazwaya kilicho mashariki mwa Mosul siku ya Jumatatu baada ya kuelekea eneo la viwanda la Kukjali.

Siku ya Jumatatu waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi, aliwaambia wanamgambo 3000 na 5000 walio ndani ya mji wa Mosul baaada ya kuuteka mwezi Juni mwaka 2014, kuwa hakuna njia ya kukimbia kwa hivyo ni afadhali wasalimu amri au wafe.

Waandishi kadhaa wanaoeandamana na vikosi hivyo wanasema kuwa majeshi ya Iraq yanakabiliwa na upinzani mkali katika vita hivyo vya kujaribu kudhibiti mji wa Mosul.

Wadadisi wanasema ikiwa majeshi ya Iraq yafanikiwa kuwa na ngome ndani ya mji wa Mosul, itakuwa mafanikio makubwa kwa Iraq na nchi zingine zote ambazo zimeshiriki kwenye vita dhidi ya kundi la Islamic State.