SYRIA-IS-USALAMA

Waasi wa Syria watangaza vita vya kuukomboa mji wa Raqqa

Wapiganaji wa kundi la Syria Democratic Forces (SDF) katika jimbo la Raqqa, nchini Syria.
Wapiganaji wa kundi la Syria Democratic Forces (SDF) katika jimbo la Raqqa, nchini Syria. REUTERS/Rodi Said

Waasi wa Syria wa kundi la Syrian Democratic Forces (SDF) wametangaza siku ya Jumapili kuanzishwa kwa mashambulizi ya mjini Raqqa, ngome kuu ya wanajihadi wa kundi la Islamic State (IS) kaskazini mashariki mwa Syria.

Matangazo ya kibiashara

Operesheni hii, iliyoanza Jumamosi usiku kwa mujibu wa muungano wa waasi wa Kiarabu na Wakurdi wanaosaidiwa na Marekani, operesheni ambayo inakuja baada ya operesheni nyingine iliyozinduliwa hivi karibuni na vikosi vya Iraq na Wakurdi wa Iraq kwa kuuweka chini ya himaya yao mji wa Mosul kaskazini mwa Iraq.

"Uongozi wa juu wa waasi wa Syria wa SDF umetangaza kuzindua kampeni yake kabambe ya kijeshi ya kuukomboa mji wa Raqqa," amesema Jehan Sheikh Amadi, msemaji wa SDF, katika mkutano na waandishi wa habari mjini Ain Rissa, kilomita sitini kaskazini mwa mji wa Raqqa.

Operesheni inayojulikana kwa jina la "Hasira ya Moto", imeanzishwa kwa uratibu wa muungano unaopambana dhidi ya kundi la IS uliyoanzishwa na Marekani, uongozi wa juu wa wa waasi wa SDF umeelezea katika taarifa yake.

Operesheni hii inalenga "kuutenga na kuuteka mji mkuu wa ugaidi wa kimataifa," taarifa hiyo ambayo haikutoa maelezo zaidi imeongeza.

Waasi wa SDF pia wameshauri raia wanaoishi katika mji wa Raqqa kuepuka maeneo waliopo wapiganaji wa kijihadi na kuelekea "maeneo huru".