ISRAEL

Vikosi vya kigeni vyaisaidia Israel kudhibiti moto unaoenea Haifa

Moto ukiteketeza misiti na makazi kwenye mji wa Haifa, Novemba 24, 2016.
Moto ukiteketeza misiti na makazi kwenye mji wa Haifa, Novemba 24, 2016. AHMAD GHARABLI / AFP

Kundi la kwanza la ndege za kigeni za zimamoto, limeanza kuisaidia nchi ya Israel kukabiliana na moto mkubwa uliozuka kwenye misitu ya nchi hiyo, ambapo umesababisha maelfu ya raia kukimbia nyumba zao.

Matangazo ya kibiashara

Wakikabiliana na moto huo kwa siku ya nne mfululizo kwenye maeneo mengi ya nchi, Serikali ya Israel iliahidiwa kusaidiwa ndege maalumu zinazotumiwa kuzima moto kutoka Urusi, Ufaransa, Uturuki, Cyprus, Ugiriki, Italia na Croatia.

Ardhini, kikosi cha zimamoto cha Palestina usiku wa kuamkia leo kiliungana na kile cha Israel, ambapo ilituma magari manne yenye nguvu ya kusukuma maji kaskazini mwa mji wa Haifa na kwenye vijiji vingine vinne ambako moto huo unaelekea jirani na Jerusalem.

Katika eneo linalokaliwa na wayahudi wengi, zaidi ya familia 400 zilihamishwa na vikosi vya Palestina na Israel.

Moto huo umeripotiwa angalau kupungua nguvu siku ya Ijumaa licha ya upepo mkali, licha ya kuwa mamlaka zimeonya kuwa huenda moto huo ukashika kasi tena wakati wowote.

Wakazi wengi kwenye mji wa Haifa walilazimika kulala nje ya nyumba zao nyakati za usiku huku wengine maelfu wakiondolewa kwenye njia ambayo moto huo unaelekea.

Mamia ya nyumba na maelfu ya misiti imeharibiwa vikali na moto huo, ambao umechangiwa pia na hali mbaya ya hewa pamoja na ukame ulioikumba nchi hiyo, hali ambayo inafanya zoezi la uokoaji kuwa gumu zaidi.