ISRAEL-PALESTINA-USHIRIKIANO

Israel yaidhinisha ujenzi wa nyumba katika Jerusalem ya Mashariki

Makazi ya Wayahudi ya Har Homa katika Jerusalem ya Mashariki, yaliyojengwa katika eneo linalojulikana kama Jabal au Maount Abu Ghneim tarehe 9 Desemba 2009.
Makazi ya Wayahudi ya Har Homa katika Jerusalem ya Mashariki, yaliyojengwa katika eneo linalojulikana kama Jabal au Maount Abu Ghneim tarehe 9 Desemba 2009. AFP / Ahmad Gharabli

Manispaa ya Israel ya mji wa Jerusalem imeidhinisha Jumatano hii, Desemba 28 ujenzi wa jengo lenye ghorofa nne kwa walowezi katika kitongoji cha Palestina katika eneo la Jerusalem ya Mashariki, muda mfupi kabla ya hotuba ya waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry, kwa mujibu wa shirika lisilo la kiserikali la Israel.

Matangazo ya kibiashara

Mradi huu unahusu kata ya Silwan iliyoko karibu na mji wa zamani wa Jerusalem. Mapema, kamati ya manispaa ya mji wa Jerusalem iliahirisha zoezi la kupiga kura juu ya ujenzi wa baadhi ya nyumba 500 katika vitongoji vingine vya eneo la Jerusalem ya Mashariki, linalokaliwa na na Waisrael, imesema Ir Amim, shirika lisilo la kiserikali la Israel linalopinga ukoloni.

Hatua hiyo inakuja siku kadhaa baada ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuitaka Israel kukomesha mara moja ujenzi wa makaazi kwa walowezi wa kiyahudi katika ardhi ya Palestina.

Inaarifiwa kuwa uamuzi huo umechukuliwa baada ya ofisi ya waziri mkuu kuiandikia kamati hiyo barua, ikisema kuwa ujenzi huo utazidisha zaidi uhasama kati ya Washington na Israel.
Wakati huo huo rais mteule wa Marekani Donald Trump ameiambia Israel kukaa imara hadi pale atakapochukua mamlaka mwezi ujao.

Zaidi ya Wayahudi 500,000 wanaishi katika makaazi 140 yaliojengwa na Israel tangu uvamizi wake 1967 ambapo walikalia maeneo ya West Bank na mashariki mwa Jerusalem.
Makaazi hayo sio halali kulingana na sheria ya kimataifa, japokuwa Israel inapinga hilo.