Hollande: Ni wajibu wetu kuwadhibiti IS ndani na nje
Imechapishwa:
Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, amesema kuwa, kuunga mkono operesheni za kijeshi dhidi ya kundi la Islamic State ni jambo la muhimu sana katika kuzuia mashambulizi ya kigaidi nyumbani, kauli aliyotoa akiwa ziarani nchini Iraq.
Rais Hollande amewahi kutembelea nchi hiyo mwaka 2014 na anabaki kuwa kiongozi mashuhuri duniani kutembelea Iraq toka ilipoanzishwa vita dhidi ya kundi hilo miaka miwili iliyopita, operesheni inayoshirikisha muungano wa nchi za kiarab.
Rais Hollande ambaye ameambatana na waziri wa ulinzi Jean-Yves Le Drian, wametembelea pia eneo la kaskazini la wakurdi linalojitegemea kiutawala kwenye ziara hii ya siku moja.
"Kuchukua hatua dhidi ya ugaidi hapa Iraq ni sawa na kuzuia matukio mengine ya kigaidi kwenye ardhi yetu," amesema haya wakati akiwa kwenye kambi ya jesho linalobambana na ugaidi jirani na mji mkuu Baghdad.
Ufaransa ni nchi ya pili kuchangia katika operesheni inayoongozwa na Marekani, ambayo mpaka sasa imetekeleza maelfu ya mashambulizi ya anga dhidi ya ngome za IS kwenye nchi za Syria na Iraq.
Majeshi ya Iraq yalionekana kuelemewa punde tu baada ya wapiganaji wa kijihadi kufanikiwa kuuchukua mji wa Mosul mwezi Juni mwaka 2014.
Toka Ufaransa ijiunge kwenye operesheni hiyo na Marekani mwezi Septemba 2014, ndege za Ufaransa zimetekeleza mashambulizi ya anga zaidi ya elfu 1 na kuharibu zaidi ya ngome elfu 1 700 za IS.