ISRAEL

Mahakama yamkuta na hatia mwanajeshi wa Israel aliyemuua raia wa Palestina

Mwanajeshi mmoja wa Israel ambaye alifyatua risasi na kumuu raia wa Palestina aliyekuwa amejeruhiwa na hakuwa na nia yoyote ya kumdhuru mwanajeshi huyo, amekutwa na hatia ya kosa la mauaji bila kukusudia, hukumu ambayo kwa kiasi kikubwa imeigawa nchi.

Mwanajeshi wa Israel, Elor Azaria akiwa mahakamani Januari 4, 2017 wakati akisomewa hukumu ya kosa la kuua bila kukusudia.
Mwanajeshi wa Israel, Elor Azaria akiwa mahakamani Januari 4, 2017 wakati akisomewa hukumu ya kosa la kuua bila kukusudia. REUTERS/Heidi Levine/Pool
Matangazo ya kibiashara

Mwanajeshi huyo, Elor Azaria, kesi yake imekuwa ikisikilizwa kwenye mahakama ya kijesho toka mwezi May mwaka jana, huku wanasiasa wa mrengo wa kulia wakionekana kumtetea licha ya viongozi wa juu wa jeshi kukosoa kitendo cha mwanajeshi huyo.

Adhabu dhidi ya mwanajeshi huyu inatarajiwa kutolewa katika siku chache zijazo, huku adhabu ya juu ya kosa alilotenda ikiwa ni kifungo cha miaka 20 jela.

Jaji kanali Maya Heller alitumia zaidi ya saa mbili na nusu kusoma uamuzi wa mahakama hiyo, akikosoa utetezi wa mawakili wa Azaria.

Kwa niaba ya majaji watatu, jaji Heller amesema hakukuwa na sababu yoyote kwa Azaria kufyatua risasi huku akijua fika raia huyo wa Palestina hakuwa hatari tena.

Hata hivyo Azaria ambaye alionekana mwenye furaha wakati akiingia mahakamani hapo, alibadilika sura wakati jaji Heller alipokuwa akisoma uamuzi wa majaji wenzake watatu.

Familia yake na marafiki walionekana kuduwazwa na uamuzi wa mahakama hiyo, ambapo mama mzazi wa mwanajeshi huyo alisikika akitamka "Unapaswa kujisikia aibu" matamshi aliyoyaelekeza kwa jaji Heller ambaye hukumu yake imekosolewa.

Azaria alikuwa na umri wa miaka 19 wakati akitekeleza mauaji hayo dhidi ya raia wa Palestina mwezi Machi 2016 katika mji wa Hebron, eneo la ukingo wa magharibi.

Maelfu ya raia wameandamana kupinga uamuzi wa mahakama ya kijeshi, huku jeshi likisema Azaria sio mtoto wa taifa na kwamba kitendo alichokifanya, alikifanya wakati akiwa mwanajeshi na kuna sheria za kijeshi.

Wanasiasa pia wamegawanyika pakubwa ambapo baadhi wanamuunga mkono Azaria na kitendo alichokifanya huku wengine wakiunga mkono uamuzi wa mahakama.