ISRAEL

Israel: Netanyahu atoa wito kwa mwanajeshi aliyeshtakiwa kupewa msamaha

Sajenti Elor Azaria, akikumbatiwa na familia yake baada ya kukutwa na hatia ya mauaji, Januari 4, 2017, Israel.
Sajenti Elor Azaria, akikumbatiwa na familia yake baada ya kukutwa na hatia ya mauaji, Januari 4, 2017, Israel. REUTERS/Heidi Levine/Pool

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ametoa wito wa kupewa msamaha kwa mwanajeshi aliyepatikana na hatia ya mauaji ya raia wa Palestina kwa kumpiga risasi wakati akiwa tayari amejeruhiwa. 

Matangazo ya kibiashara

Elor Azaria, ambaye kesi yake katika mahakama ya kijeshi tayari imeigawa nchi hiyo toka mwezi May ilipoanza, alikutwa na hatia Jumatano ya Januari 4, huku wanasiasa wa mrengo wa kushoto wakimtetea licha ya uongozi wa jeshi la nchi hiyo kudai kuwa kitendo chake kilienda kinyume na maadili ya jeshi hilo.

Kufuatia uamuzi huu wa mahakama, Azaria sasa atakabiliwa na kifungo cha miaka 20 jela.

Akuzungumzia uamuzi huo wa mahakama, waziri mkuu Netanyahu ametoa wito kwa mwanajeshi huyo mwenye asili ya Israel na Ufaransa, kusamehewa.

"Ulikuwa ni wakati mgumu sana na unaoumiza kwetu sote, lakini zaidi ni kwa Elor na familia yake," Aliandika Netanyahu kupitia mtandao wake wa kijamii wa Facebook.

Waziri mkuu wa Israel, Benyamin Netanyahu.
Waziri mkuu wa Israel, Benyamin Netanyahu. REUTERS/Gali Tibbon/Pool

"Naunga mkono kusamehewa kwa Elor Azaria."

Waziri mkuu Netanyahu, pia hata kabla ya kesi yenyewe kuanza, tayari alimuita kwenye ikulu yake, baba mzazi wa Azaria na kumueleza masikitiko yake.

Awali ofisi ya rais Reuven Rivlin ilisema wazi kuwa, mazungumzo yoyote kuhusu kusamehewa kwa mwanajeshi huyo sio wakati muafaka sasa na kwamba mazungumzo hayo yanaweza kufanyika mara baada ya mchakato wote wa kimahakama kumalizika.

Mahakama hiyo ya kijeshi huenda ikatoa adhabu rasmi kwa mwanajeshi huyo, mwishoni mwa juma, na baada ya hapo upande wa utetezi unaweza kukata rufaa.

Jaji kiongozi kwenye kesi hiyo, Maya Heller, alitumia muda wa saa mbili na nusu kusoma uamuzi wa mahakama, huku akikosoa vikali utetezi wa upande wa mawakili wa Azaria, aliosema haukuwa na mashiko.