UTURUKI

Uturuki: Watu zaidi wakamatwa kuhusiana na tukio la kwenye klabu ya usiku ya Reina

Maua na picha za waliouawa katika shambulio la klabu ya usiku ya Reina, zikiwa zimewekwa nje ya geti la klabu hiyo.
Maua na picha za waliouawa katika shambulio la klabu ya usiku ya Reina, zikiwa zimewekwa nje ya geti la klabu hiyo. REUTERS/Osman Orsal

Kikosi maalumu cha polisi nchini Uturuki kimewakamata watu kadhaa kwa tuhuma za kuhusika katika shambulio la kwenye klabu moja ya usiku mjini Istanbul, ambako watu 39 waliuawa, wakati huu mamlaka nchini humo zikizidisha msako na kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya mipaka.

Matangazo ya kibiashara

Kikosi maalumu kimefanya msako maalumu Alhamisi ya tarehe 5 Januari, na kuwakamata watuhumiwa zaidi wanaodaiwa kuhusika kwenye shambulio hilo wakati wa mkesha wa kuamkia mwaka mpya.

Ripoti za kukamatwa kwa watu zaidi zimechapishwa katika jarida la Serikali na kwamba operesheni hizo zilifanyika kwenye maeneo ya Uighur linalokaliwa na watu wenye asili ya kutoka Xinjiang China.

Polisi wanadai walipokea taarifa za siri zikieleza kuwa kuna uwezekano mkubwa ya kuwepo kwa watu waliohusika kwenye mipango ya utekelezaji wa shambulio hilo.

Ukiondoa tukio la kukamatwa kwa watu hawa, zaidi ya watu 36 wamekamatwa hadi sasa na wanachunguzwa, lakini mtuhumiwa mkuu wa shambulio lenyewe bado hajapatikana baada ya kufanikiwa kuwatoroka polisi baada ya tukio.

Mamlaka nchini humo zimeimarisha pia ulinzi kwenye maeneo ya mipaka ya nchi yake kwa hofu kuwa huenda kuna watu wakajaribu kutoroka.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu, Jumatano ya wiki hii alitangaza vyombo vya usalama kumbaini muhusika wa shambulio hilo bila kutoa taarifa zake zaidi.

Kati ya watu 39 waliouawa kwenye tukio hilo, watu 27 walikuwa ni raia wa kigeni kutoka Lebanon, Saudi Arabia, Israel na Morocco.