UN-PALESTINA-ISRAEL-USHIRIKIANO

Nchi 70 kutafutia ufumbuzi wa pamoja mzozo wa Israel na Palestina

Picha ya washiriki katika Mkutano wa mjini Paris kuhusu  Mashariki ya Kati, Januari 15, 2017.
Picha ya washiriki katika Mkutano wa mjini Paris kuhusu Mashariki ya Kati, Januari 15, 2017. REUTERS/Bertrand Guay

Wajumbe katika mkutano wa Kimataifa kujadili amani kati ya Israel na Palestina, wamezitaka pande hizo mbili kuacha kuchukua misimamo mikali wakati huu juhudi za kufufua mazungumzo ya amani zikiendelea.

Matangazo ya kibiashara

Wajumbe hao walikutana Jumapili mwishoni mwa juma hili lililopita jijini Paris nchini Ufaransa katika mkutano ambao umekaribishwa na Palestina lakini Israel imeonekana kutokuwa na imani na juhudi za mataifa 70 yanayijaribu kufufua mazungumzo hayo.

Washiriki katika mkutano huo kuhusu amani katika Mashariki ya Kati walisema katika mji wa Paris katika tamko la mwisho dhamira yao ya suluhu kwa mataifa hayo mawili katika mgogoro kati ya Israel na Palestina na kutoa wito kwa Waisrael na Wapalestina "kuonyesha nia yao ya ufumbuzi katika mzozo kati ya mataifa hayo mawili, na kujiepusha na hatua au kitendo kitakachochukuliwa na upande mmoja kuhusu masuala ya mipaka, mji wa Jerusalem na wakimbizi, " huku wakiongeza kuwa kama vitendo hivyo vitachukuliwa, "hawatavitambua. "

Nakala, iliyotolewa baada ya mkutano huo kati ya wajumbe kutoka nchi 70 na mashirika ya kimataifa, haijaeleza wazi kuhusu mapendekezo ya utawala mpya wa Marekani, hasa nia ya rais mteule wa Marekani Donald Trump ya kuhamisha ubalozi wa Marekani nchini Israeli katika mji wa Jerusalem.

Mapema mchana, Rais wa Ufaransa François Hollande alisisitiza kwamba "suluhu kwa mataifa mawili, ambayo jumuiya ya kimataifa ilikua ilifikia kwa miaka kadhaa, inaonekana kutishiwa."

Viongozi wa nchi kadhaa za kiarabu, nchi za Ulaya na nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameshiriki katika mkutano huo.

Hata hivyo Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hawakushiriki katika mkutano huo, baada ya serikali ya Kiyahudi kusem kile ilichokiita mkutano ulioliwa kimakosa.