SYRIA-MAZUNGUMZO

Mazungumzo ya amani kuhusu Syria yang'oa nanga mjini Astana

Waandishi wa habari wakirekebisha vyombo vyao kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya amani ya Syria.
Waandishi wa habari wakirekebisha vyombo vyao kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya amani ya Syria. REUTERS/Mukhtar Kholdorbekov

Waasi nchini Syria Jumatatu hii wanakutana na viongozi wa Serikali ya Damascuss, kwenye mazungumzi yanayofanyika mjini Astana, Kazakhistan, yakiwa ni mazungumzo mengine yanayijaribu kumaliza vita nchini Syria.  

Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo hayo yameanza saa tano asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki, na yanatarajiwa kuwa ni mazungumzo ya mara ya kwanza ambayoyatawakutanisha ana kwa anapande zinazohasimiana toka kuanza kwa vita nchini humo mwaka 2011.

Mazungumzo haya yamekaribishwa kwa mikono miwili na pande zote zinazohusika kwenye mzozo huo, huku wawakilishi kutoka pande zote waliwasili mjini Astana wakiwa na mtazamo tofauti kuhusu mazungumzo yenyewe.

Tayari kumeibuka hofu ya pande hizo kufikia makubaliano kutokana na namna wajumbe wa pande zote mbili wameeleza misimamo tofauti kuelekea mazungumzo haya.

Kwenye mazungumzo haya, wajumbe watajadiliana namna mazungumzo hayo yatakavyoendeshwa ili kuzisaidia pande zote mbili kuelewa mazingira na kile ambacho kitazungumzwa kwa siku zote watakazokuwa huko.

Waasi wanasema mazungumzo yao yatajikita katika kutafuta makubaliano ya kusitisha mapigano kitaifa kwa miezi kadhaa, mpango ambao ni wazi umeonekana kuungwa mkono na utawala wa rais Assad na ule wa Uturuki.

Hata hivyo utawala wa rais Assad unasisitiza kwanza waasi hao waweke silaha chini kwa kupewa msamaha wa kutoshtakiwa na Serikali pamoja na kutoa wito wa kupatikana kwa suluhu ya kisiasa ili kumaliza vita iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya laki 3.

Mazungumzo haya yanaratibiwa na Uturuki, Iran na Urusi, yanakuja ikiwa ni miezi kadhaa imepita toka majeshi ya Serikali yafanikiwe kuuchukua mji wa Aleppo.

Mpatanishi mkuu wa upinzani Mohammed Alloush aliwasili mjini Astana siku ya Jumapili akiambatana na maofisa kadhaa  kutoka upande wa waasi.