SYRIA-UNSC

UN: China, Urusi zatumia kura ya turufu kukwamisha azimio la vikwazo dhidi ya Syria

Naibu balozi wa Urusi kwenye baraza la usalama la umoja wa Mataifa, Vladmir Safronkov akinyanyua mkono kupiga kura ya turufu kuzuia azimio la vikwazo dhidi ya Syria, 1 Machi 2017.
Naibu balozi wa Urusi kwenye baraza la usalama la umoja wa Mataifa, Vladmir Safronkov akinyanyua mkono kupiga kura ya turufu kuzuia azimio la vikwazo dhidi ya Syria, 1 Machi 2017. REUTERS/Mike Segar

Nchi za Urusi na China zimetumia kura yao ya turufu kuzuia azimio la umoja wa Mataifa lililoungwa mkono na nchi za Magharibi, azimio ambalo lingeshuhudia kutangazwa kwa vikwazo vipya dhidi ya Syria kutokana na tuhuma za matumizi ya silaha za kemikali.

Matangazo ya kibiashara

Mjadala wa kuiwekea nchi ya Syria vikwazo kutokana na tuhuma za utawala kutumia silaha za kemikali, umekuwa ni wa kwanza kufanyika kwenye baraza la usalama tangu kuingia madarakani kwa rais mpya wa Marekani, Donald Trump.

Kura hii ya VETO iliyotumiwa na nchi za China na Urusi, imekuja wakati huu mazungumzo ya amani ya mjini Geneva, yakiwa hayaoneshi dalili yoyote ya kupiga hatua kuelekea kumaliza vita vilivyodumu nchini Syria kwa zaidi ya mika 6 sasa.

Hii ni mara ya saba kwa utawala wa Moscow, mshirika wa karibu wa kijeshi kwa nchi ya Syria kutumia kura ya turufu kuulinda na kuutetea utawala wa Damascus. China yenyewe hii ni mara ya sita kutumia kura yake kuutetea utawala wa Bashar al-Assad.

Rais wa Urusi Vladmir Putin awali kabla ya kufanyika kwa kura hiyo, alionya kuwa kutangaza vikwazo dhidi ya Syria wakati huu sio jambo la busara ukitilia maanani kwamba kuna mazungumzo yanayoendelea kujaribu kumaliza vita nchini humo.

Balozi wa Marekani kwenye baraza la usalama, Nikki Halet hata hivyo alitupilia mbali madai ya Urusi na kusisitiza kuwa azimio hili la vikwazo limekuja wakati muafaka.

Balozi Nikki aliongeza kuwa "ni siku ya huzuni kwa baraza la usalama pale unapoona nchi nyingine zinatafuta sababu kutetea mauaji yanayotekelezwa kwa raia wake."

Azimio hili lilipendekezwa na nchi ya Uingereza, Ufaransa na Marekani lilipata kura 9 peee, huku nchi tatu zilizopinga azimio hilo zilikuwa ni Bolivia, China na Urusi. Misri, Ethiopia na Kazakhstan zenyewe hazikupiga kura.

Kwa azimio lolote la umoja wa Mataifa kupitishwa, linahitaji kura 9 za turufu na kusiwe na kura yoyote ya turufu kupinga azimio hilo.