GENEVA-SYRIA

Ujumbe wa Serikali ya Syria yawashutumu upinzani kwa kutaka kuyateka mazungumzo

Kiongozi wa ujumbe wa Serikali ya Syria kwenye mazungumzo ya Geneva, Bachar al-Jaafari.
Kiongozi wa ujumbe wa Serikali ya Syria kwenye mazungumzo ya Geneva, Bachar al-Jaafari. FABRICE COFFRINI / AFP

Ujumbe wa Serikali ya Syria unaoshiriki mazungumzo ya amani mjini Geneva, unalituhumu kundi la upinzani kwa kuyaweka mazungumzo hayo mateka, kauli inayotolewa wakati huu mazungumzo hayo yakielekea katika saa za mwisho. 

Matangazo ya kibiashara

Ujumbe wa Serikali unasema utawawajibisha upinzani ikiwa mazungumzo haya hayatatoka na muafaka wowote kumaliza vita vilivyodumu kwa karibu miaka 6 sasa.

Baada ya juma moja la mazungumzo ya kando, hakuna dalili zozote za pande hizo mbili kukutana ana kwa ana.

Tuhuma hizi zinatishia kuvunjika kwa makubaliano ya usitishaji wa mapigano, na huku kukiwa hakuna dalili za uwezekano wa viongozi hao kuafikiana kuhusu namna watakavyofanya mazungumzo kabla ya kufikia tamati kwa mkutano huu.

"Hatupaswi kukubali jukwaa la Riyadh kuyateka mazungumzo haya," amesema kiongozi wa ujumbe wa Syria, Bashar al-Jaafari wakati akizungumza na wanahabari baada ya kukutana na msuluhishi mkuu Staffan de Mistura.

Jaafari ameongeza kuwa suala hili halikuja kwao kwa mshangao kwa sababu baadhi ya wajumbe wa Riyadh unahusisha pia viongozi wa makundi ya kigaidi.

Katika mazungumzo yake na wanahabari ambayo hakuyafanya kwa zaidi ya siku tatu, Jaafari ameutuhumu ujumbe wa upinzani wenye makao yake Saudi Arabia kukataa kuwajumuisha makundi mengine madogo kwenye muungano wao.

Hatua pekee kwenye mazungumzo haya imegubikwa na mivutano kutoka kwa pande hizo mbili hasa kuhusu uundwaji wa ujumbe wa upinzani na uwezekano wa kujumuishwa kwa makundi ya kigaidi kwenye mazungumzo hayo.