SYRIA-USALAMA

Rubani wa MiG-23 asema ndege yake ilidunguliwa

Mabaki ya MiG-23, ndege ya serikali ya Syria iliyodunguliwa kwenye mpaka na Uturuki, Jumamosi  Machi 4, 2017.
Mabaki ya MiG-23, ndege ya serikali ya Syria iliyodunguliwa kwenye mpaka na Uturuki, Jumamosi Machi 4, 2017. REUTERS

Rubani wa MIG-23, ndege ya jeshi la Syria iliyodunguliwa Jumamosi kwenye mpaka wa Uturuki amewambia viongozi wa Uturuki kwamba ndege yake ilidunguliwa, wakati ambapo alikua anaenda kushambulia jimbo la Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria, shirika la habari la serikali la Anatolia limearifu.

Matangazo ya kibiashara

Rubani, ambaye alinusurika baada ya kufaulu kuondoka ndani ya ndege hiyo ikiwa angani, alipatikana kwa msaada wa timu ya waokoaji kutoka Uturuki na amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Hatay.

Ndege yake iliondoka mapema Jumamosi katika mji wa Latakia, kaskazini magharibi mwa Syria kabla ya kudunguliwa katika jimbo la Idlib, alisema rubani huyo.

Rubani huyo, ambaye ana umri wa miaka 56, anasumbuliwa na majeraha, hasa katika uti wa mgongo, hali ya afya yake haiko hatarini, alisema msemaji wa hospitali.