Kundi la IS lakiri kuhusika na shambulio kwenye hospitali ya kijeshi Kabul
Imechapishwa:
Watu wenye silaha waliovalia mavazi ya matabibu wa hospitali, wamevamia hospitali kubwa ya kijeshi kwenye mji wa Kabul nchini Afghanistan, shambulizi ambalo kundi la kiislamu la Islamic State limekiri kuhusika.
Makabiliano yanayoendelea kwenye hospitali ya Sardar Daud Khan, ymesababisha vifo vya watu watatu mpaka sasa na wengine 66 wamejeruhiwa, huku milipuko na milio ya risasi vikiendelea kusikika kwenye mtaa ambao wanakaa pia wanadiplomasia wa kimataifa.
Wauguzi na wafanyakazi wengine wa hospitali wamejificha kwenye vyumba vya hospitali wakiandika ujumbe wa kuomba msaada kupitia kwenye mitandao ya kijamii, huku televisheni moja ikionesha watu walionaswa kwenye madirisha.
Uongozi wa hospitali hiyo umesema kuwa wapiganaji wenye silaha wakiwa wamevalia mavazi ya kitabibu walifanikiwa kuingia baada ya mtu mmoja kujitoa muhanga kwenye geti la kuingilia hali iliyotoa mwanya kwa watu hao kuingia ndani ya hospitali.
Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Afghanistan, Dalwat Waziri ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, wapiganaji watatu wakiwa wamejihami na silaha aina ya AK-47 na mabomu ya kutupa kwa mkono ndio waliingia kwenye eneo la hospitali.