SYRIA-MAREKANI

Marekani yatuma mitambo maalumu kwenye mji wa Raqa, Syria

Moja ya mitambo ya Marekani ambayo imepelekwa nchini Syria.
Moja ya mitambo ya Marekani ambayo imepelekwa nchini Syria. REUTERS/Khalid al Mousily

Nchi ya Marekani imetuma makomandoo pamoja na vifaa vya kurusha maroketi nchini Syria kwa lengo la kusaidia kulishinda kundi la Islamic State kwenye mji wa Raqa, mji ambao unaaminika kuwa ngome kuu ya wapiganaji hao wa kiislamu.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa maofisa wa Serikali ya Marekani, wamesema kuwa nchi hiyo imetuma vifaa zaidi ya 11 vya kijeshi kwenye eneo la mpaka na Syria.

Wanajeshi hao maalumu tayari wameanza kutekeleza operesheni kusaidia kuwakabili wapiganaji hao kwenye mji wa Raqa, taarifa zinazotolewa na kuthibitishwa baada ya kuchapishwa kwenye gaztei la Washington Post.

Uamuzi huu wa kupeleka wanajeshi ni ishara kubwa kwa nchi hiyo katika ushiriki wake wa vita dhidi ya makundi ya wanajihadi nchini Syria.

Kwa sasa nchi ya Marekani imeweka ukomo wa wanajeshi wake wa ardhini nchini Syria hadi kufikia 500, wanajeshi hao wakiwa na jukumu la kutoa mafunzo kwa wapiganaji wa jeshi huru la Syria na wale wapiganaji wa Kikurdi.

Kwa mujibu wa gazeti la The Post, uamuzi huu ulikuwa unafanyiwa kazi kwa muda sasa na haukuwa sehemu ya mahitaji ya rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump kuongeza wanajeshi zaidi nchini Syria.

Mitambo hii maalumu ya kurusha makombora, itasaidia sana wapiganaji wa jeshi huru la Syria ambao wamekuwa wakipiga hatua muhimu kuingia kwenye mji wa Raqa.

Maofisa wa Serikali ya Marekani wanakadiria kuwa kuna wapiganaji wa kijihadi zaidi ya elfu 4 kwenye mji wa Raqa, mji ambao una wakazi zaidi ya laki 3.