Unicef: Watoto wengi waliuawa mwaka 2016 nchini Syria

Mtoto raia wa Syria akiwa kwenye mji wa Manbij, Machi 7, 2017
Mtoto raia wa Syria akiwa kwenye mji wa Manbij, Machi 7, 2017 REUTERS/Rodi Said

Shirika la umoja wa Mataifa linalohusika na watoto UNICEF, linasema kuwa watoto wengi wameuawa nchini Syria mwaka 2016, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwenye mwaka wowote toka kuanza kwa vita nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Unicef inasema kuwa, watoto 652 wamekufa, 255 kati yao waliawa wakiwa shuleni mwaka uliopita, ikiwa ni ongezeko la asilimia 20 zaidi kutoka idadi ya waliokufa mwaka 2015.

Idadi hii inaelezwa kuwa ni ile idadi ambayol imethibitishwa, hali hii ikimaanisha kuwa huenda idadi ikawa ni zaidi ya inayotolewa sasa.

Shirika hilo linaamini kuwa watoto wanaofikia zaidi ya 800 walichukuliwa kwenda kujiunga na makundi ya wapiganaji mwaka 2016.

Ripoti inasema idadi hii ni mara mbili ya ile ya mwaka 2015. Huku wale waliochukuliwa kwenda kupigana, wakitumiwa kuwa mstari wa mbele na kutumiwa kama wauaji, walinzi wa magereza na kujitoa muhanga.

Mkurugenzi wa Unicef kwa nchi za mashariki ya kati, Geert Cappelaere, anasema kuwa "ukubwa wa mateso wanayoyapata hauelezeki".

"Mamilioni ya watoto nchinik Syria wanajikuta kwenye mashambulizi kila siku kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, maisha yao hayaelezeki." amesema mkurugenzi huyo.

Watoto milioni 6 hivi sasa wanategemea misaada ya kibinadamu kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, vita ambayo sasa imedumu kwa zaidi ya miaka 6.

Watoto wanaokadiriwa kufikia milioni 2 na laki 3 wamekimbia nchi yao, huku walioko kwenye hatari zaidi wakifikia milioni 2 na laki 8 na hawa wakiwa wamenaswa kwenye maeneo yenye vita kali.