URUSI-IRAN

Putin na Rouhani wakutana, mzozo wa Syria ajenda ya mazungumzo yao

Rais wa Iran, Hassan Rouhani akiwa na waziri mkuu wa Urusi Dimtry Medvedev. Tarehe 27 Machi 2017
Rais wa Iran, Hassan Rouhani akiwa na waziri mkuu wa Urusi Dimtry Medvedev. Tarehe 27 Machi 2017 Sputnik/Pool/Ekaterina Shtukina

Rais wa Urusi Vladimir Putin anakutana na mwenzake wa Iran Hassan Rouhani kwa mazungumzo mjini Moscow, mazungumzo ambayo yanatazamwa na mataifa ya magharibi kujua hatua watakazochukua kuhusu Syria.

Matangazo ya kibiashara

Ziara ya Rouhani ni ya kwanza kuifanya kwa nchi ya Syria wakati huu nchi hizo mbili zikiwa ni wafadhili wakubwa wa utawala wa Syria na wamekuwa wakijaribu kumaliza vita vilivyodumu nchini humo kwa zaidi ya miaka 6.

Kabla ya ziara hii, msemaji wa wizara ya mambo ya nje Bahram Ghasemi alisema katika ziara hii viongozi hawa wawili watazungumzia kuhusu masuala ya usalama wa ukanda na hasa kwenye nchi ya Syria na kutafuta suluhu ya kudumu pamoja na mapambano dhidi ya ugaidi.

Rouhani amesindikizwa na waziri wake wa mambo ya kigeni Mohammad Javad Zarif na waziri wa mafuta Bijan Zanganeh pamoja na maofisa wengine wa juu wa Serikali.

Viongozi hawa wanatarajia kutiliana saini mikataba zaidi ya 10 ya ushirikiano wa kiuchumi na nchi ya Urusi.

Punde baada ya kuwasili nchini Urusi, rais Rouhani alikutana na waziri mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev, huku rais Rouhani akisema anatarajia ziara hii kuwa ya mafanikio na kubadili sura ya uhusiano wa nchi hizo mbili.

Kabla ya ziara yake Serikali ya Moscow ilisema viongozi wa nchi hizo mbili watazungumzia masuala ya ushirikiano wa kiuchumi, biashara na uwekezaji.

Mbali na ushirikiano wa kibiashara na hali ya Syria, masuala ya nishati na ulinzi kati ya Iran na Urusi ni mambo yatakayojadiliwa licha ya sintofahamu zinazojitokeza kuhusu Syria.

Nchi ya Urusi imesema itajenga vinu vya nyuklia zaidi ya 20 kwaajili ya kuzalisha nishati katika kipindi cha miaka michache ijayo pamoja na kuipa Iran mtambo wake wa usalama wa s-300.

Rais Rouhani anatazama kuboresha uchumi wa nchi yake tayari kwa uchaguzi wa mwezi Mei mwaka huu ambapo anatarajia kugombea kwa muhula wa pili.