JORDAN

Wakuu wa nchi za Kiarabu wanakutana Jordan mzozo wa Syria kuwa ajenda

Mfalme wa Jordan, Abdullah II akimpokea mgeni wake mfalme wa Saudi Arabia Salman alipowasili mjini Amman. Machi 27, 2017
Mfalme wa Jordan, Abdullah II akimpokea mgeni wake mfalme wa Saudi Arabia Salman alipowasili mjini Amman. Machi 27, 2017 REUTERS/Ammar Awad

Wakuu wa nchi kutoka Jumuiya ya nchi za Kiarabu wanakutana nchini Jordan kwa mkutano wao wa mwaka huku kukiwa hakuna matarajio yoyote kwa viongozi hao kutatua mizozo inayoikumba eneo la mashariki ya kati pamoja na vita dhidi ya ugaidi.

Matangazo ya kibiashara

Mfalme wa Saudi Arabia Salman ni miongoni mwa wakuu wa nchi 22 wanaohudhuria mkutano huu.

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Antonio Guterres na mpatanishi wa mzozo wa Syria balozi Staffan de Mistura nao pia wanatarajiw akuhudhuria mkutano huu wa nchi za Kiarabu.

Viongozi wa nchi hizio wanatarajiwa kujadili vita vinavyoendelea kwenye nchi za Syria, Iraq, Libya na Yemen, vita dhidi ya ugaidi na mzozo kati ya Palestina na Israel, na hii ni kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Jordan.

Wadadi wengi wa masuala ya siasa wanaona kuwa mkutano huu hautakuwa na tofauti sana na mkutano uliopita wa wakuu hawa ambao walishindwa kuchukua hatua madhubuti kutuliza hali ya mambo kwenye ukanda wao.

Wadadisi hao wameongeza kuwa mfumo wa Jumuiya hii sio imara, viongozi wenyewe wamegawanyika na kumeshuhudiwa watu wengi wakijiweka kando kwa miaka kadhaa.

Nchi hizi 22 wanachama zimeshindwa kabisa kutatua mizozo iliyoibuka kwenye baadhi ya nchi wanachama toka mwaka 2011 wakati yalipoibuka maandamano kwenye nchi hizo kudai demokrasia ikiwemo mzozo wa Syria uliodumu kwa miaka 6 sasa.

Mkuu wa Jumuiya hiyo Abul Gheit Jumatatu ya wiki hii alitoa wito kwa viongozi hao kutoa mchango chanya utakaopelekea kumaliza mizozo inayozikumba nchi zao.

Rais wa Syria Bashar al-Assad hajaalikwa kwenye mkutano huu toka mwaka 2011 wakati kulipozuka maandamano ya kuupinga utawala wake na yeye kutumia nguvu kuwaminya wapinzani.