SYRIA

Urusi yatumia kura ya veto kuzuia azimio dhidi ya Syria

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wakipiga kura.
Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wakipiga kura. UN Photo/Loey Felipe

Urusi imetumia kura ya veto kuzuia kupitishwa kwa azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuishutumu serikali ya Syria kuhusika na shambulizi la silaha za kemikali lililosababisha vifo vya raia 80 wiki iliyopita na kuitaka  Damascus kushirikiana na wachunguzi wake ili kubaini ukweli.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii ya Urusi imelaaniwa vikali na Marekani, Uingereza na Ufaransa zilizowasilisha azimio hilo.

Hii ni mara ya kwanza  kwa Urusi kutumia kura ya veto kuzuia kupitishwa kwa azimio lolote dhidi ya Syria.

Nikki Haley Balozi wa Marekani katika Baraza hilo la Usalama amesema inashangaza ni vipi Urusi imeendela kuitetea Syria hata baada ya rais Bashar Al Assad kuagiza kutekelezwa kwa shambulizi hilo.

Marekani na Urusi zimekuwa zikilaumiana kuhusu mzozo wa Syria, huku Washington DC ikisema Moscow ilishindwa kuzuia wanajeshi wa Syria kutekeleza shambulizi hilo.

Rais Trump aliagiza kushambuliwa kwa uwanja wa ndege wa kijeshi nchini Syria na kuharibu ndege zake za kivita baada ya shambulizi hilo na kuonya kuwa, itaichukulia hatua zaidi ikiwa shambulizi lingine kama hilo litafanyika.

Trump ambaye amesema ingekuwa vema ikiwa uhusiano wa nchi yake na Urusi ungeimarika, ameeleza kuwa ni kweli kwa sasa uhusiano kati ya nchi hizo mbili umedora, kauli ambayo siku ya Jumatano ilitolewa na rais Vladimir Putin.