AFGHANISTAN-USALAMA

Zaidi ya watu 90 wauawa na 100 kujeruhiwa katika shambulio mjini Kabul

Vikosi vya usalama vya Afghanistan katika eneo la mlipuko wa bomu lililotegwa katika gari mjini Kabul Mei 31, 2017.
Vikosi vya usalama vya Afghanistan katika eneo la mlipuko wa bomu lililotegwa katika gari mjini Kabul Mei 31, 2017. AFP

Zaidi ya watu tisini waliuawa na zaidi ya 100 wengine kujeruhiwa Jumatano hii asubuhi katika mlipuko mkubwa wa bomu lililotegwa katika gari katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, Wizara ya Afya imesema.

Matangazo ya kibiashara

Polisi ilithibitisha kwamba mlipuko huo ulitokea karibu na ubalozi wa Ujerumani, katika eneo ambapo kunapatikana ofisi mbalimbali na majengo muhimu ya serikali.

"Ilikuwa bomu lililotegwa katika gari karibu na ubalozi wa Ujerumani, lakini pembezoni mwa eneo la tukio kuna majengo muhimu na ofisi kadhaa. Ni vigumu kusema nani alikua amelengwa," alisema msemaji wa polisi mjini Kabul, Basir Mujahid.

Zaidi ya watu 100 waliojeruhiwa walisafirishwa hospitalini katika mji wa Kabul, alisema msemaji wa Wizara ya Afya na kuongeza kuwa idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka.

Moshi mweusi ulitandaa eneo la kati la mji wa Kabul na nyumba zilizo kwenye mita kadhaa kutoka eneo la mlipuko zimeharibiwa.

Hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo. Msemaji wa kundi la Taliban amesema bado anachunguza.