IRAN-SAUDI ARABIA-MVUTANO

Iran: watu waliokamatwa na Saudia si wanajeshi wa Iran

Abbas Ali Cadkhodai, msemaji wa Baraza kuu la kitaifa la Ulinzi nchini Iran,katika mkutano na waandishi wa habari  katika Grand Hotel mjini Tehran, Mei 17,2017
Abbas Ali Cadkhodai, msemaji wa Baraza kuu la kitaifa la Ulinzi nchini Iran,katika mkutano na waandishi wa habari katika Grand Hotel mjini Tehran, Mei 17,2017 Jan van der Made

Iran imekana kuwa watu watatu waliokamatwa na kikosi cha wanamaji wa Saudia siku ya Ijumaa wiki iliopita sio wanajeshi wake na badala yake kubaini kwamba watu hao ni wavuvi tu ambao walikua wakifanya kazi yao ya uvuvi.

Matangazo ya kibiashara

Watu hao walikamatwa na Saudia Arabia wakati boti yao ilipokuwa ikiwasili karibu na ufukwe mmoja wa bahari ulio na mafuta na kusema kuwa ni wanachama wa jeshi la Iran.

Hata hivyo kitengo cha habari cha Saudia kimetangaza kuwa shambulio la kigaidi katika eneo hilo la mafuta limetibuliwa na kubaini kwamba jeshi lake linaendelea na operesheni zake na kukagua maeneo kadhaa ambayo yanalengwa kushambuliwa na Iran katika ardhi yake.

Afisa mkuu wa maswala ya mipakani kweye wizara ya mambo ya ndani nchini Iran Majid Aghababaie, amewaambia waandishi wa habari kwamba utambulisho wa watu hao unajulikana na kwamba hakuna ushahidi kwamba walikuwa wanajeshi.

Vita vya maneno kati ya Saudia Arabia na Iran vimeendelea kushuhudiwa siku za hivi karibuni katika ukanda huo. Itafahamika kwamba nchi hizi mbili hasimu zenye Waislamu kutoka madhehebu mawili makubwa katika dini ya Uislamu zimekua zikihasimiana kila upande ukilaumu mwengine kujihusisha na vitendo vya ugaidi.