SYRIA-IS-USALAMA

Watu zaidi ya 30 waangamia katika mapigano Deir Ezzor, Syria

Gari la kundi la wapiganaji la FDS mashariki mwa Deir Ezzor, Septemba 12, 2017.
Gari la kundi la wapiganaji la FDS mashariki mwa Deir Ezzor, Septemba 12, 2017. REUTERS/Rodi Said

Watu thelathini na tano, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, wameuawa Jumanne hii, Septemba 12, katika mapigano karibu na mji wa Deir Ezzor, mashariki mwa nchi mwa Syria.

Matangazo ya kibiashara

Idadi ya watu ambao wameuawa ndani ya siku nne imefikia 90, katika mashambulizi ya angani yanayoshtumiwa kutekelezwa na ndege za Urusi, lakini pia ndege za muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani.

Vifo hivi vinatokea wakati ambapo kundi la Islamic state linakabiliana na mashambulizi mawili tofauti dhidi ya ngome yake ya mwisho nchini Syria. mashambulizi ya kwanza yanaendeshwa magharibi mwa mkoa huo kwenye ukingo wa kulia wa Eufrate na jeshi la serikali ya Syria, likisaidiwa na washirika wake wa Hezbollah kutoka Lebanon na jeshi la Urusi. Katika siku chache tu, majeshi haya yalisonga mbele kilomita 100 jangwani, kurejesha kwenye himaya yao kilomita mraba 4,000 kutoka mikononi kundi la IS na kuvunja uzio uliyowekwa kwa miaka mitatu katika maeneo mawili ya serikali.

Kwa upande wa mashariki mwa jimbo hilo, kwenye ukingo wa kushoto wa mto, muungano wa wapiganaji wa Kiarabu na Wakurdi walizindua operesheni kabambe, bila kushirikiana na askari wa serikali. Wapiganaji wa kundi la SDF, wakisaidiwa na Marekani, wamefika kilomita sita kutoka ukingo wa mto upande wa mkoa wa Deir Ezzor unaokaliwa na wapiganaji wa kundi la IS.

Mbio kwa ajili ya udhibiti wa eneo la mashariki mwa Syria zimeanza. Jeshi la serikali imetuma kikosi cha askari ili kuendelea na mashambulizi yake. Msafara mrefu wa magari na vifaa vya kijeshi vimeonekana vikiingia katika mkoa wa Deir Ezzor. Lengo la jeshi la Syria ni kuvuka mto ili kuzuia barabara kwa vikosi vya wapiganaji wa Kiarabu na wakurdi na kuwazingira wapiganaji wa kundi la IS katika mji huo.