PALESTINA-HAMAS-FATAH-USALAMA

Hamas na Fatah kupatia ufumbuzi tofauti zao

Msafara wa Waziri Mkuu wa Palestina Rami Hamdallah uliwasili katika Ukanda wa Gaza siku ya Jumatatu kwa ziara ya kuimarisha upatanisho na Hamas, ambayo inadhibiti eneo hilo kwa miaka kumi.
Msafara wa Waziri Mkuu wa Palestina Rami Hamdallah uliwasili katika Ukanda wa Gaza siku ya Jumatatu kwa ziara ya kuimarisha upatanisho na Hamas, ambayo inadhibiti eneo hilo kwa miaka kumi. REUTERS/Amir Cohen

Vyama viwili vikubwa vya siasa vya Palestina, Fatah na Hamas vimepiga hatua katika kusuluhisha tofauti baina yao iliyodumu kwa muongo mmoja, baada ya ziara iliyofanywa na Waziri mkuu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Matangazo ya kibiashara

Hivi karibuni Rami Hamdallah aliuambia umati wa maelfu ya watu kwamba wakati umefika sasa kumaliza mgawanyiko miongoni mwa Wapalestina.

Msemaji wa kundi la wapiganaji wa Palestina, amesema kuwa maelezo ya makubaliano yatatangazwa katika mkutano na vyombo vya habari mjini Cairo, ambapo awamu ya pili ya mazungumzo ya upatanishi yataanza siku ya Jumanne.

Mwezi uliopita chama cha Hamas kilikubaliana kuvunja utawala wao ukanda wa Gaza kwa ajili ya kupisha serikali ya muungano na chama cha Fatah kinachoongozwa na Waziri mkuu Hamdallah, ambacho makao yake ni Ukingo wa magharibi.

Akizungumzia hilo, kwa upande wake mjumbe wa Umoja wa Mataifa ukanda wa Gaza Nickolay Mladenov amesema serikali mpya ya Gaza imeweza kubeba majukumu yake, hali inayotia matumaini kwamba shida za kibinadamu zitapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Mapema mwezi Oktoba kundi la Hamas lenye mamlaka yake huko Gaza, lilisema linataka kuanza majadilano na wapinzani wao Fatah, ambao wana nafasi kubwa katika mamlaka inayoongozwa na rais Mahmoud Abbas huko upande wa Ukingoni magharibi kwa lengo la kutaka kuunda serikali ya muungano.

Mwezi Septemba taarifa rasmi ya Hamas ilisema itaanza kwa kuivunja kamati yake ya utawala wa Gaza na kisha kuitisha uchaguzi mkuu.

Hatua hiyo inafuatia mazungumzo baina ya viongozi wa Hamas na maafisa wa ngazi ya juu kutoka Misri.

Kundi la Fatah kwa upande wao wamesema wanakaribisha hatua hiyo.

Tangu mafarakano ya hapo 2007, wakati ambapo Hamas ilishinda uchaguzi wa eneo hilo, hatua mbalimbali zimechukuliwa kujaribu kupatanisha pande hizo mbili bila mafanikio.

Hamas wanatambuliwa kama kundi la kigaidi na Israel, Marekani, Muungano wa nchi za Ulaya, Uingezea na mataifa mengine.

Tangu mwaka 2007 Israel na Misri wameweka vizuizi vya ardhini na hewani kwa ukanda wa Gaza kwa lengo la kuzuia mashambulizi kwa wanamgambo wa Gaza.