LEBANON-HEZBOLLAH-USALAMA

Hezbollah yakanusha kutuma silaha kwa nchi za Kiarabu

Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah akitoa hotuba yake kwenye televisheni, Beirut, Jumatatu, Novemba 20, 2017.
Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah akitoa hotuba yake kwenye televisheni, Beirut, Jumatatu, Novemba 20, 2017. REUTERS/ Jamal Saidi

Kiongozi wa Hezbollah kutoka Lebanon, ambaye chama chake kilishtumiwa siku ya Jumapili na Umoja wa nchi za Kiarabu kama kundi la kigaidi, amekanusha kutuma silaha katika nchi za Yemen, Bahrain na Kuwait.

Matangazo ya kibiashara

Hassan Nasrallah amesema kuwa Hezbollah iliikomba Lebanon kutoka uvamizi wa Israel na ilichangia kushindwa kwa kundi la Islamic State nchini Syria na Iraq.

Bw. Nasrallah amefutilia mbali shutma za ugaidi dhidi ya chama chake iliotolewa siku ya Jumapili usiku na Umoja wa nchi za Kiarabu, akitaja tuhuma hizo kwamba ni za "ajabu" na "ujinga." Hassan Nasrallah ameshtumu kauli hiyo ya kwamba Hezbollah ni kundi la kigaidi " wakati ambapo iliukomboa mji wa Syria wa Abu Kamal kutoka mikononi mwa kundi la Islamic State," huku akitetea Iran kushtumiwa kudhamini ugaidi "wakati ambapo inasaidia katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa kijihadi ".

Hezbollah pia iliikomboa Lebanon kutoka mikononi mwa Israeli na inaendelea kulinda nchi hiyo dhidi ya vitisho kutoka kwa Wayahudi, Bw. Nasrallah alisema.

Pia alisisitiza jukumu la chama chake katika kushindwa kwa wanamgambo wa Kiislamu nchini Iraq na Syria, akitangaza kwamba washauri wake na maafisa wa kijeshi wanaweza kuondoka nchini Iraq wakati serikali ya Baghdad itatangaza kushindwa kwa kundi la Islamic State.

Kwa mujibu wa Hassan Nasrallah, uongozi (ukhalifa) uliotangazwa na IS umevunjwa. Lakini hiyo haimaanishi kuwa kundi hilo halipo tena. Wapiganaji wake wamekimbilia katika maeneo ya jangwa la Syria na Iraq.

Pia alikanusha kuwa Hezbollah ilihusika kwa urushaji wa kombora la masafa marefu mapema mwezi Novemba lililorushwa na waasi wa Yemen dhidi uwanja wa ndege wa Riyadh.

Nasrallah alisema "silaha za Hezbollah ni muhimu katika kulinda utulivu Lebanon".