LEBANON-HEZBOLLAH-USALAMA

Saad Hariri arejea Lebanon

Waziri Mkuu wa Lebanon alietangaza kujiuzulu Saad Hariri.
Waziri Mkuu wa Lebanon alietangaza kujiuzulu Saad Hariri. REUTERS/Mohamed Azakir

Saad Hariri yuko nchini Lebanon tangu siku ya Jumanne usiku, karibu wiki tatu baada ya kuitumbukiza nchi yake katika mgogoro mpya wa kisiasa baada ya kutangaza kujiuzulu kwenye nafasi yake ya waziri mkuu nchini Saudi Arabia.

Matangazo ya kibiashara

Bw. Hariri aliwasili Beirut akitokea Cyprus baada ya Cairo ambako alikuwa na mazungumzo mafupi na rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi, vyombbo vya habari vya serikali nchini Misri vimearifu.

Saad Hariri alikuwa Paris tangu siku ya Jumamosi, ambapo alikutana na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. Alitangaza kuwa atakua nchini Lebanon hadi siku ya Jumatano, katikahali ya kusherehekea sikukuu ya kitaifa.

Baada ya kuondoka Cairo, alielekea Cyprus kwa mazungumzo na rais Nicos Anastasiades, amesema msemaji wa ikulu ya Cyprus.

Kujiuzulu kwake wakati wa hotuba iliyorushwa kwenye televisheni nchini Saudi Arabia, alisababisha mgogoro mkubwa wa kisiasa kuzuka nchini Lebanon, huku vita vya maneno vikienelea kati ya Saudi Arabia na Iran.

Rais wa Lebanon, Michel Aoun, ambaye anaungwa mkono na Hezbollah, bado hajakubali rasmi kujiuzulu kwa Saad Hariri akisema anasubiri arejee nchini ili kujadili suala hilo.

Ikiwa Saad Hariri atathibitisha kujiuzulu kwake, Michel Aoun ataomba Bunge kuteua mtu mwengine atakae jaza nafasi hiyo.