ISRAEL-UN-MAREKANI-PALESTINA-USHIRIKIANO

Guterres: uamuzi wa Trump juu ya Israel unachochea vurugu

Waandamanaji wa Wapalestina wakichoma moto picha inayoonyesha rais wa Marekani Donald Trump na bendera ya Marekani wakati wa maandamano dhidi ya uamuzi wa Trump kutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel katika mji wa Gaza tarehe 7 Desemba 2017.
Waandamanaji wa Wapalestina wakichoma moto picha inayoonyesha rais wa Marekani Donald Trump na bendera ya Marekani wakati wa maandamano dhidi ya uamuzi wa Trump kutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel katika mji wa Gaza tarehe 7 Desemba 2017. REUTERS/Mohammed Salem

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hatua ya rais Trump kuutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel inaleta sintofahamu katika juhudi za kuleta amani katika mzozo wa Israel na Palestina a hivyo kusababisha mvutano mkubwa kati ya nchi za Kiarabu na Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Mapema wiki jana siku moja baada ya rais wa Marekani Donald Trump kuweka wazi hatua yake ya kuutambiua mji huo kama makao makuu ya Israel, kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mamoud Abbas alifutilia mbali mazungumzo kati yake na Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence, ambae kwa upande wake ameshtumu uamuzi huo wa kiongozi wa Palestina.

Siku ya Jumapili akihutubia umati wa watu Recep Tayyip Erdogan aliielezea Israeli kama "nchi ya kigaidi" ambayo "inaua watoto", huku akiongeza kuwa "atapambana kwa njia zote" dhidi ya Jerusalem kutambuliwa na Marekani kama mji mkuu wa Israel.

"Palestina inatelekezwa na kufanyiwa madhila mbalimbali wakati haina hatia (...) Lakini Israeli, ni nchi kigaidi, ndiyo, nchi ya kigaidi!", Erdogan alisema wakati wa hotuba yake katika mji wa Sivas, katikati mwa Uturuki. "Hatutaacha Jerusalem kwa maslahi ya serikali inayoua watoto," Bw Erdogan aliongeza.

Hayo yanajiri wakati ambapo maandamano yanaendelea katika nchi mbalimbali za Kiarabu kupinga hatua hiyo ya Marekani kutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Wakati huo huo kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis alisema Jerusalem ni mji mtakatifu kwa wakristo,Wayahudi na Waislam.

Amesema ni mazungumzo pekee yanayoweza kuleta suluhu katika mzozo huo wa Irael na Palestina.

Jumuiya ya kimataifa imeendela kukosoa hatua ya rais wa Marekani kuhusu Israel, ikibani kwamba hatua hiyo itaendelea kuchochea machafuko katika nchi hizi mbili.