PALESTINA-ISRAEL-USALAMA

OIC yatangaza kutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Palestina

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) yatangaza kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Palestina.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) yatangaza kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Palestina. /REUTERS/Kayhan Ozer

Jumuiya ya nchi za Kiislamu (OIC), ambayo iimekutana leo Jumatano katika mji wa Istanbul, nchini Uturuki, imelaani na kufutilia mbali uamuzi wa rais Donald Trump kutambua Jerusalem kama mji mkuu wa taifa la kiyahudi.

Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa ya pamoja, Jumuiya ya nchi za Kiislamu OIC inaona kwamba mpango wa Marekani unaonyesha jinsi gani nchi hiyo imeshindwa na kujiondoa moja kwa moja katika jukumu lake kama mpatanishi katika mchakato wa amani katika Mashariki ya Kati.

Jumuiya ya nchi za Kiislamu imetangaza katika taarifa hiyo kwamba"Jerusalem ya Mashariki ni mji mkuu wa taifa la Palestina" na "imetoa wito kwa nchi zote kutambua taifa la Palestina na Jerusalem ya Mashariki kama mji mkuu wa wa taifa hilo".

Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, alielezea mpango wa Marekani kama "uhalifu mkubwa" ambao unakiuka sheria ya kimataifa na kutishia kugeuza mapambano ya kisiasa katika mapambano ya kidini.

Aliomba rasimu ya azimio iwasilishwe kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kutangaza uamuzi wa Donald Trump hauna nguvu yoyote.

"Jerusalemu daima itabaki kuwa mji mkuu wa Palestina," Mahmoud Abbas alisema.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan pia aliomba jumuiya ya kimataifa kutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Palestina na kumwomba Rais wa Marekani kutafakari upya uamuzi ambao, kwa maoni yake, unaonyesha tu "vitendo vya ugaidi" vinavyofanywa na Israel.

"Tunatolea wito nchi zote zinazounga mkono sheria ya kimataifa kutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Palestina inayokaliwa kimabavu na Israel, hatuwezi kusubiri tena," Erdogan alisema. "Israeli ni taifa linalokalia kimabavu Palestina, Israeli ni taifa la kigaidi" ameongeza Erdogan, rais wa Uturuki.