SYRIA-UN-USALAMA

UN kuchunguza madai ya matumizi ya silaha za kemikali Syria

Raia wakikimbilia maeneo salama baada yamashambulizi ya angani, Douma katika jimbo la Ghouta Mashariki mnamo Februari 6, 2018.
Raia wakikimbilia maeneo salama baada yamashambulizi ya angani, Douma katika jimbo la Ghouta Mashariki mnamo Februari 6, 2018. REUTERS/ Bassam Khabieh

Umoja wa Mataifa umesema unachunguza taarifa kuwa silaha za kemikali zilitumika kushambulia maeneo yanayokaliwa na waasi nchini Syria wakati huu nchi ya Urusi ikitumia kura yake ya turufu kuzuia azimio la baraza la usalama kulaani shambulio hilo.

Matangazo ya kibiashara

Watalaam wa Umoja wa Mataifa wamesema, waanachunguza ripoti ya jeshi la serikali ya Syria kutumia silaha za kemikali dhidi ya wapinzani wa serikali.

Hata hivyo, serikali ya Syria imekanusha madai hayo.

Tume ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia uchunguzi wa masuala ya haki za binadamu nchini Syria imeeleza kuwa imepokea ripoti zinazodai kuwa silaha hizo zilitumika katika maeneo hayo.

Tume hiyo imefafanua kuwa inazichunguza taarifa za ripotti hizo ambazo zimedai kuwa silaha za mabomu ya kemikali za chlorine zilitumika katika mji wa Saraqeb kwenye jimbo la Idlib na mjini Douma katika jimbo Ghouta.

Wakazi wa mji wa Ghouta Karibu na mji mkuu, Damascus pamoja na wakazi wa jimbo la Idlib katika wiki za hivi karibuni wamekuwa wakituhumu makundi yenye silaha kuwa yanatumia silaha za sumu.

Katika hatua nyingine Marekani imesema kuwa kuna ushahidi wa wazi wa kutumika kwa silaha hizo za gesi ya chlorine katika maeneo mbalimbali nchini Syria likiwemo eneo hilo la Ghouta linaloshikiliwa ma waasi.

Idadi ya watu waliouawa siku ya Jumanne imefikia sasa 47, wakiwemo watoto 10.

Watu zaidi ya laki tatu na elfu arobaini wameuawa tangu kuzuka kwa mgogoro wa Syria mwaka 2011 kwa kuanzia na maandamano ya kupinga utawala wa Rais Bashar Al Assad ambayo baadaye yaligeuka na kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.