PALESTINA-URUSI-USHIRIKIANO

Abbas kuzuru Urusi kupata uungwaji mkono dhidi ya Marekani

Vladimir Putin na Mahmoud Abbas,wakati wa mkutano wao Sochi, Mei 11, 2017.
Vladimir Putin na Mahmoud Abbas,wakati wa mkutano wao Sochi, Mei 11, 2017. REUTERS/Yuri Kochetkov/Pool

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas anatarajiwa kufanya ziara ya kiserikali nchini Urusi leo Jumatatu, wiki mbili baada ya ziara ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Lengo la ziara ya Abbas nchini Urusi ni kuhakikisha anapata uungwaji mkono wa Urusi kutoka kwa vyadimir Putin dhidi ya Marekani kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israeli.

Awali mkutano wa viongozi hawa wawili uliopangwa kufanyika katika mji wa Sochi, utafanyika katika mji wa Moscow kwa sababu ya ajali ya ndege iliyoanguka na kuua watu 71 siku ya Jumapili karibu na mji mkuu wa Urusi, kwa mujibu wa ikulu ya Kremlin.

Ziara hii inakuja siku mbili baada ya mfululizo wa mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya maeneo kadhaa ya Syria na Iran katika kile kinachoelezwa na Israel kama ulipizaji kisasi, kutokana na ndege isio na rubani ya Iran iliyoingia kwenye anga yake.

Vladimir Putin na Benjamin Netanyahu walizungumza kwa simu baada yamashambulizi hayo. Rais wa Urusi alionya dhidi ya kutokea kwa hali ya "hatari" nchini Syria wakati ambapo Benjamin Netanyahu alisema kuwa Israeli "itaendelea kushambulia wale wote wanaojaribu kutushambulia au kutuvamia".

Mahmoud Abbas, ambaye anakataa mawasiliano yoyote na utawala wa Rais Donald Trump tangu Marekani kutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel mwishoni mwa mwaka 2017, anatazamia kutoa hotuba yake mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 20 Februari.

Wapalestina wanaona kuwa uamuzi wa Marekani unapinga madai yao kuhusu Jerusalem ya Mashariki iliyovamiwa na kushikiliwa kimabavu na Wayahudi.

Akituhumiwa na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, kutokua na utashi wa kufikia makubaliano ya amani na Israel, Abbas amekataa upatanishi wowote na Marekani katika kutatua mgogoro kati ya Israel na Palestina na ameahidi watu wake kuwa atafanya kilio chini ya uwezo wake ili taifa la Palestina litambuliwe na Umoja wa Mataifa.