UTURUKI-SYRIA-USALAMA

Askari 31 wa Uturuki wapoteza maisha katika vita Syria

Askari wa Uturuki katika mkoa wa Bersaya, kaskazini mwa mji wa Syria wa Azaz, karibu na mpaka na Uturuki, Januari 23, 2018.
Askari wa Uturuki katika mkoa wa Bersaya, kaskazini mwa mji wa Syria wa Azaz, karibu na mpaka na Uturuki, Januari 23, 2018. AFP

Askari thelathini na mmoja wa Uturuki wameuawa na 143 wamejeruhiwa tangu kuanza kwa mashambulizi ya jeshi la Ankara kaskazini magharibi mwa Syria, uongozi wa jeshi la Uturuki umebaini leo Jumatatu. Tangazo hili linakuja siku mbili baada ya Uturuki kupoteza askari wake.

Matangazo ya kibiashara

Tangu kuanza kwa operesheni hiyo tarehe 20 Januari, "ndugu zetu 31 walikufa ni mashujaa, 143 walijeruhiwa," uongozi wa jeshi la Uturuki limeandika kwenye tovuti yake.

Uturuki ilianza mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi kutoka kundi la wapiganaji la YPG, kundi ambalo Uturuki inalichukulia kama la "kigaidi" lakini linasaidiwa na Marekani dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu kutoka kundi la Islamic State (IS ).

Vita, kwa upande mmoja, kati ya jeshi la Uturuki na washirika wake wa Kiarabu kutoka Syria , na upande wa pili, kundi la waasi la YPG vinaendelea katika eneo la Afrin, ngome ya wapiganaji wa Kikurdi, kaskazini magharibi mwa Syria.

Jeshi la Uturuki limepata hasara kubwa katika siku za hivi karibuni, bila hata hivyo kusonga mbele. siku ya Jumamosi, askari 11 wa Uturuki waliuawa, ikiwa ni pamoja na helikopta moja iliyoharibiwa vibaya.

Wakati huo huo wapiganaji wasiopungua 165 kutoka makundi ya Kiarabu yanayosaidiwa na Uturuki wameuawa tangu kuanza kwa mashambulizi hayo, kwa mujibu wa shirika la Haki za Binadamu nchini Syria la OSDH.

Jeshi la Uturuki pia limesema leo Jumatatu kuwa limewaangamiza mpaka sasa "magaidi" wasiopungua 1,369,idadi ambayo ni vigumu kuchunguza na kubwa ikilinganishwa na ile iliyotolewa na OSDH. Hivi karibuni shirika hili lilibaini kwamba wapiganaji 152 wa kundi la waasi la YPG waliuawa.