SYRIA-MAUAJI-USALAMA

Zaidi ya watu 100 waangamia katika mashambulizi Ghouta Mashariki

Kijiji cha Mesraba, katika eneo hilo linalozingirwa na linashikiliwa na waasi wa Ghouta Mashariki, karibu na Damascus, Syria, mnamo Februari 19, 2018.
Kijiji cha Mesraba, katika eneo hilo linalozingirwa na linashikiliwa na waasi wa Ghouta Mashariki, karibu na Damascus, Syria, mnamo Februari 19, 2018. AFP/Hamza Al-Ajweh

Watu wasiopungua 100, ikiwa ni pamoja na watoto 20, waliuawa mnamo Februari 19 katika mashambulizi makubwa ya jeshi la Syria dhidi ya eneo la Ghouta mashariki linaloshikiliwa na waasi, karibu na Damascus, kwa mujibu wa shirika la haki za binadamu nchini Syria, OSDH.

Matangazo ya kibiashara

Watu zaidi ya 300 walijeruhiwa katika mashambulizi hayo angani, kwa mujibu wa shirika hilo lenye makao yake nchini Uingereza.

Wakazi wa eneo la Ghouta mashariki anaendelea kuyatoroka makazi yao, huku wengine wakiwa na wasiwasi wa kushambuliwa na majeshi ya Syria. Televisheni ya Siria imesema kuwa jeshi la Syria limekua likilenga ngome za "magaidi", neno linalotumiwa na vyombo vya habari vya serikali kubainisha waasi na wapoiganaji wa kijihadi.

Mashambulizi haya mapya yanakuja baada ya siku mbili za utulivu, huku kukiwa na mazungumzo kati ya serikali na waasi, ambao wanashikilia eneo hili kubwa lililozingirwa na majeshi ya serikali. Watu takriban 400,000 bado wanaishi katika eneo al Ghouta mashariki. Lakini Mohammad Allouche, kiongozi wa Jaych al-Islam, kundi kubwa la waasi huko Ghouta, amekanusha kuepo kwa mazungumzo na serikali ya Damascus.

Mkurugenzi wa shirika lai haki za binadamu nchini Syria (OSDH), Rami Abdel Rahman, amesema kuwa makombora 300 yalianguka katika eneo la Ghouta pamoja na mashambulizi kadhaa ya angani. Roketi kadhaa zilizorushwa na waasi zilianguka katika mji mkuu na kuwajeruhi watu kadhaa.

Serikali ya Bashar al-Assad imeamua kuendelea na mashambulizi kwa lengo la kurejesha kwenye himaya ya serikali Ghouta ya Mashariki.