PALESTINA-AFYA-USALAMA

Mahmoud Abbas aruhusiwa kutoka hospitali ya Baltimore

Rais wa Mamlaka ya Palestina mbele ya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Rais wa Mamlaka ya Palestina mbele ya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. REUTERS/Lucas Jackson

Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, ambaye amekua akifanyiwa vipimo vya matibabu katika hospitali ya Baltimore nchini Marekani, aliruhusiwa kutoka hospitali jana Alhamisi usiku, ambapo alikua amelazwa, afisa wa ngazi ya juu nchini Palestina amesema.

Matangazo ya kibiashara

Afisa huyo, ambaye amesema kiongozi wa Palestina anaendelea vizuri, huku ameongeza kuwa Bw Abbas anatarajiwa kurudi Ramallah katika Ukingo wa Magharibi leo Ijumaa.

Awali ilikua ilipangwa kuwa angelifanya ziara ya kikazi nchini Venezuela kutoka Marekani, kwa mujibu wa ofisi yake. Ziara hii ingelianza siku ya Jumatano.

Abbas mwenye umri wa miaka 82, alizungumza siku ya Jumanne mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa huko New York, na aliomba mkutano wa kimataifa katikati ya mwaka huu kufufua mchakato wa amani kati ya Israeli na Palestina.

Mahmoud Abbas alichukua hatamu ya uongozi wa nchi ya Palestina baada ya kifo cha mtangulizi wake Yasser Arafat mwaka 2004. Aliendeleza mazungumzo ya amani na Israeli, lakini mazungumzo yalivunjika mwaka 2014 na hayajaanza tena tangu wakati huo.