UN-SYRIA-USALAMA

Umoja wa Mataifa kuchukua uamuzi kuhusu mapigano Syria

Mapigano yaendelea kurindima Ghouta mashariki, Februari 21, 2018.
Mapigano yaendelea kurindima Ghouta mashariki, Februari 21, 2018. REUTERS/Bassam Khabieh

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajia kukutana leo Ijumaa kupiga kura juu ya muswada wa azimio kuhusu usitishwaji wa mapigano kwa muda wa siku 30 nchini Syria.

Matangazo ya kibiashara

Muswada huo unalenga kuruhusu kusafirishwa kwa misaada ya kibinadamu katika eneo la mapigano na kuwaondoa watu waliojeruhiwa na wagonjwa.

Tangazo hili lilitolewa na balozi wa Kuwait katika Umoja wa Mataifa, ambaye ni mwenyekiti wa mwezi huu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mpaka sasa msimamo wa Urusi, mshirika wa Syria, haujulikani. Urusi ambaye ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa anaweza kutumia kura yake ya turufu, kwa kupinga azimio hilo.

Tangu kuanza kwa mgogoro nchini Syria, mgogoro ambao unaingia sasa mwaka wa nane, Urusi ambayo iliingia kijeshi nchini humo mnamo mwaka 2015 katika kusaidia vikosi vya Syria vinavyunga mkono serikali, imetumia kura yake ya turufu mara kumi na moja kupinga rasimu za maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa Syria.

Rasimu ya azimio inapaswa kupata kura tisa na sio kutokabiliwa na kura ya turufu kutoka kwa mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalam la Umoja wa Mataifa (Urusi, China, Marekani, Uingereza na Ufaransa).

Siku ya Alhamisi ndege za kivita ziliendesha mashambulizi katika eneo linaloshikiliwa na waasi Ghouta mashariki, karibu na Damascus, kwa siku tano mfululizo. Mashambulizi haya ya jana ni miongoni mwa mashambulizi mabaya tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa nchini Syria walitoa wito mapema mwezi Februari kusitishwa mapigano mara moja angalau kwa muda wa mwezi mmoja ili kusafirisha misaada ya kibinadamu katika maeneo ya mapigano.