SYRIA-MAPIGANo-USALAMA

Mapigano yaendelea kurindima Ghouta Mashariki

Mlipuko wakati wa mashambulizi ya angani ya majeshi ya serikali ya Syria, Februari 23, 2018 Ghouta mashariki.
Mlipuko wakati wa mashambulizi ya angani ya majeshi ya serikali ya Syria, Februari 23, 2018 Ghouta mashariki. Ammar SULEIMAN / AFP

Kundi la waasi linastumu majeshi ya serikali ya Syria kutumia gesi ya klorini wakati wa mashambulizi yao katika eneo la Ghouta mashariki. Madai ambayo yamefutiliwa mbali na Urusi ambayo ni mshirika mkuu wa serikali ya Syria.

Matangazo ya kibiashara

Wakazi wa Ghouta mashariki wanaendelea kusubiri kuanza kutekelezwa mkataba wa kusitisha mapigano uliopendekezwa na Umoja wa Mataifa mapema wiki hii iliyopita.

Eneo la Ghouta mashariki limeendelea kwa siku kadhaa kukumbwa na mashambulizi ya angani yanayoendeshwa na majeshi ya Syria na yale ya washirika wa serikali ya nchi hiyo Urusi. Mashambulizi hayo yamewaua watu zaidi ya 500 kwa wiki moja pekee.

Wakati huo huo maafisa wa Afya nchini Syria katika maeneo ya waasi yaliyozingirwa kaskazini mwa Ghouta wamesema watu kadhaa wamedhurika kutokana na na dalili zinazoonesha kuathiriwa na gesi ya Klorini, wakati wa mashambulizi yaliyokuwa yakifanywa na majeshi yanayounga mkono serikali.

Mashambulizi ya ardhini yalipamba moto jana Jumapili, licha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusimamishwa kwa mapigano hayo.

Mapema wiki hii iliyopita Umoja wa Mataifa ulipiga kura azimio la kubebea msaada wa chakula katika eneo ala Ghouta mashariki na kutaka pande zinazohasimiana kusitisha mapigano kwa muda wa siku thelathini.