URUSI-MAREKANI-SYRIA-USALAMA

Marekani na Urusi washambuliana kuhusu Syria

Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, New Yok, Aprili 10, 2018.
Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, New Yok, Aprili 10, 2018. REUTERS/Brendan McDermid

Urusi na Marekani wameshambuliana katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu utaratibu wa kuchunguza matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria.

Matangazo ya kibiashara

Tangu siku ya Jumamosi, mvutano mkali unaendelea katika ngazi ya kidiplomasia ya kimataifa, baada ya mashambulizi ya kemikali yanayodaiwa kutekelezwa na majeshi ya Syria dhidi ya mji wa Douma. Viongozi wa nchi za Magharibi wameendelea kupendekeza hatua ya kijeshi ichukuliwe dhidi ya utawala wa Bashar al-Assad.

"Urusi imepuuzia uaminifu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa," alisema Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Nikki Haley. Ni "ujanja," aliongeza, "historia itakumbusha kwamba leo, Urusi imechagua kuonyesha uhasama badala ya maisha ya watu wa Syria. "

"Unachukua hatua nyingine kuelekea makabiliano," alimwambia mwenzake wa Urusi Vassily Nebenzia, wakati ambapo Marekani inatishia kutumia nguvu kuadhibu mashambulizi ya siku ya Jumamosi, yanayodaiwa kutekelzwa na majeshi ya serikali ya Syria.

Kwanza, Urusi ilipinga kwa kutumia kura yake ya turufu kwa rasimu ya Marekani iliyopendekeza kuundwa kwa "Tume huru ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa" (Unimi) kuhusu matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria. Rasimu ya azimio ya Marekani iliungwa mkono na kura kumi na mbili, nchi mbili zilipiga kura dhidi ya rasimu hiyo - Urusi na Bolivia - na China ilijizuia.

Kwa upande wake,Urusi iliwasilisha rasimu ya azimio iliyolenga kusaidia uchunguzi wa Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) katika mji wa Douma nchini Syria. Rasimu hiyo ilipigiwa kura na nchi tano tu. Nchi nne zilipigia kura dhidi ya rasimu hiyo ya Urusi na sita zilijizuia.

Siku ya Jumanne serikali ya Syria ilitoa wito kwa OPCW (Shirika la Kuzuiaji Silaha za Kemikali) kutuma wakaguzi katika mji wa Douma, ngome ya mwisho ya waasi mashariki mwa Ghoutakaribu na Damascus. "Timu hiyo inajiandaa kutuma ujumbe wake nchini Syria kwa siku za usoni," imesema OPCW, ambayo mamlaka yake ni kuchunguza madai ya mashambulizi, lakini haina jukumu la kutambua wahusika.

Ufaransa yapendekeza hatua ya kijeshi

Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia, alishtumu Marekani, Ufaransa na Uingereza kuchochea mvutano wa kimataifa kwa "sera yao ya kukabiliana" dhidi ya Urusi na Syria. "Wanatishia Urusi kwa njia zisizokubalika na kauli wanazotoa zinapita kile kinachokubalika. Hatujawahi kuona kitu kama hicho, hata wakati wa vita vya baridi, "Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa alisema.

Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May waalisema katika mazungumzo ya simu siku ya Jumanne kuwa hawataruhusu mashambulizi ya kemikali kuendelea nchini Syria, kwa mujibu wa Ikulu ya White House.

Mjini London, Ofisi ya waziri mkuu wa Uingereza (Downing Street) imeripoti kuwa Theresa May alizungumza kwa nyakati tofauti na marais wa Marekani na Ufaransa na kwamba viongozi hao watatu walisisitiza haja ya kuchukua hatua ya kimataifa kwa mashambulizi ya kemikali yaliyotekelezwa katika mji wa Douma siku ya Jumamosi.

Ufaransa itatangaza "katika siku zijazo", kwa ushirikiano na Marekani na Uingereza, uamuzi wake kuhusu uwezekano wa hatua ya kijeshi dhidi ya "mashambulizi ya kemikali" ya utawala wa Syria na "washirika" wake Urusi na Iran, alisema siku ya Jumanne Rais Emmanuel Macron.